Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Vyombo vya Habari Vyatakiwa Kuzibeba 4R za Falsafa ya Rais Samia
Dec 10, 2023
Vyombo vya Habari Vyatakiwa Kuzibeba 4R za Falsafa ya Rais Samia
Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Mobhare Matinyi akizungumza leo Desemba 10, 2023 jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Umoja wa Vyama vya Waandishi wa Habari Tanzania.
Na Lilian Lundo - MAELEZO

Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Mobhare Matinyi amevitaka Vyombo vya Habari nchini kubeba falsafa  ya R4 (Reconciliation, Resilience, Reforms na Rebuilding) ili kuipeleka nchi mahali ambapo nchi nyingine zitabaki kushangaa.

Bw. Matinyi amesema hayo leo Desemba 10, 2023 jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Umoja wa Vyama vya Waandishi wa Habari Tanzania.

“Vyombo vya Habari vinaweza kuzibeba 4R za Falsafa ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu  na tukazitumia kwenda mahali ambapo nchi nyingine zitabaki zinashangaa,” amesema Bw. Matinyi.

Ameendelea kusema kuwa Rais Samia Suluhu amekuja na Falsafa ya R4. Ametaja R ya kwanza  ambayo ni “Reconciliation” yaani maridhiano au upatanisho, kuwa ni muhimu kwa makundi yote yanayosigana.

“Nchi yetu ina migogoro mingi, kama migogoro ya ardhi, lakini ukisafiri unaweza kujiuliza kwa nini tuna migogoro ya ardhi wakati tuna nchi kubwa hivi; Kwa hiyo Waandishi tunapaswa kuangalia kweli tuna sababu ya kuwa na migogoro katika nchi hii? Rais Samia hapendi migongano anataka tukae katika utaratibu,” amesema Bw. Matinyi.

Akizungumzia kuhusu R ya pili “Resilience” yaani ustahimilivu, ametoa mfano katika tukio la Hanang’ ambapo amesema kuwa, katika tukio hilo si tu Wananchi wameonyesha ustahimilivu, lakini hata watu waliokwenda pale kama vile Askari ambao wamefika katika eneo lenye changamoto lakini wameweza kukaa kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa eneo hilo. Ikiwa ni alama ya upendo kwa wananchi wenzao, na kwa ajili ya nchi yao.


Aidha ameielezea R ya tatu “Reforms” yaani mageuzi kwa kusema, “tunapozungumza kuhusu uchumi wa vyombo vya habari, tunazungumzia kwenda kwenye mageuzi. Tusikubali leo ikawa kama jana, na jana kama juzi, lazima kesho yetu ionyeshe kwamba tulivuna kitu leo kilichotokana na tulichovuna jana, twende tupige hatua mbele”.

Amefafanua kuwa, nchi yetu ina mambo inayafanya, ambayo ni mageuzi ya kipekee. Mfano sera ya elimu mpya imekuja, ambapo sasa hivi mtu ana uhakika wa kusoma mpaka chuo kikuu, kwani mwanafunzi anapomaliza kidato cha Sita ana uhakika wa kupata mkopo kuendelea na elimu ya juu.

“Haya yote yanaweza kutusaidi kufanya R ya nne “Rebuild” ya kujenga taifa letu. Uandishi ni chachu ya kufanya mambo haya yote, mfano kilichoibeba filamu ya Royal Tour ni Sekta ya Habari nje ya nchi na hapa Tanzania,” amesema Bw. Matinyi.

Ameongeza kwa mujibu wa Mwenyekiti wa TATO (Tanzania Association of Tour Operators) ni kuwa Tanzania imevunja rekodi ya mwaka 2019 ambao ndio ulikuwa mwaka bora kwa utalii katika historia ya nchi. Amesema kuwa mwaka huu utakapoisha utaweka namba kubwa, ambao mwakani hawatakuwa na shida ya kuipita. Amesema wameshamalizana mpaka na watalii watakaokuja mwakani mwezi wa Sita.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi