Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. William Lukuvi ametoa rai kwa Vyama vya Siasa kumtumia yeye kama daraja la kufikisha serikalini mawazo au maoni yatakayo chochea maendeleo.
Kauli hiyo ya Waziri Lukuvi ameitoa wakati akifungua kikao cha dharura cha Baraza la Vyama vya Siasa kinachofanyika mjini Dodoma chini ya Mwenyekiti wake Juma Khatibu. Kikao hicho cha dharura kimeitishwa ili kujadili hali ya siasa nchini kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024.
Waziri Lukuvi amesema kuwa, uzoefu wake bungeni chini ya mfumo wa vyama vingi na ushiriki wake kwenye masuala mbalimbali tokea mwaka 1995 unamfanya kuwa mmoja wao na ametoa rai kwa viongozi wa vyama hivyo vya siasa kudumisha amani, maelewano na maendeleo kwa sababu vyama hivyo ni moja ya nyenzo ya kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.
"Mkiwa na mambo yenu ambayo mnaona mnaweza kushiriki niambieni tu, mimi ni waziri wa siasa hivyo mkiwa na shughuli zenu huko kwenye majimbo mkinialika nakuja, nataka tujenge umoja na tuelewane” amesisitiza Waziri Lukuvi.
Waziri Lukuvi amesema nia yake ni kufungua milango ya ushirikiano kwa kuvifanya vyama vyama vya siasa kuwa karibu na serikali sio tu kwenye masuala ya siasa hata yale ya maendeleo. Ameongeza kuwa, serikali inaongozwa na Chama Cha Mapinduzi lakini inayo wajibu wa kushirikiana na vyama vingine vya siasa kwa sababu serikali imewekwa na watu wenye itikadi zinazotofautiana.
Kuhusu utayari wa serikali kupokea masuala yatakayojadiliwa kwenye kikao hicho Waziri Lukuvi amelihakikishia baraza hilo kuwa serikali imejiandaa kuyapokea mapendekezo yote na kuyapatia utatuzi mapema iwezekanavyo.