Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Viwanja Zaidi ya 4000 Vyapimwa Katika Makazi Holela Dar Es Salaam
Jun 20, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na Jonas Kamaleki.

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imepima viwanja 4333 hadi mwishoni mwa Mei, 2017 ambapo hatua za umilikishaji zimeanza kutekelezwa ili kurasimisha maeneo yaliyojengwa kiholela jijini Dar es Salaam.

Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Mipango Miji na Vijiji wa Wizara hiyo, Bertha Mlonda katika maohojiano maalum na mwandishi wahabari hii.

Kwa mujibu wa Mlonda, jumla ya viwanja 6,000 vinatarajiwa kupimwa na kumilikishwa katika jiji la Dare es Salaam katika zoezi zima la urasimishaji wa makazi holela.

“Pamoja na urasimishaji katika Jiji la Dar es Salaam, halmashauri nyingine 6 zimepangwa kutekeleza mradi huo. Halmashauri hizo ni; Manispaa za Musoma, Kigoma-Ujiji, Tabora, Singida, Sumbawanga na Lindi”, amesema Mlonda.

Aidha, Mlonda amesema kuwa mradi unatekelezwa katika Kata za Kimara na Saranga Manispaa ya Ubungo ambazo zina ukubwa wa hekta 3,960.8. Kata ya Kimara, inajumuisha mitaa sita (6) ambayo ni Kilungule “A”, Kilungule “B”, Mavurunza, Baruti, Kimara Baruti na Golani. Kata ya Saranga ina jumla ya mitaa saba (7) ambayo ni Kimara B, King’ong’o, Matangini, Michungwani, Saranga, Stopover na Upendo.

Ameongeza kuwa kwa pamoja kata hizo zina wastani wa viwanja 34,000 ambapo mradi umeanza kutekelezwa katika Kata ya Kimara kwenye Mitaa ya Kilungule ‘A’, Kilungule ‘B’ na sasa Mavurunza. Lengo la Mradi ni kutambua, kupanga, kupima na kumilikisha viwanja 6,000.

Mkurugenzi Msaidizi huyo amesema kuwa baada ya kukamilisha michoro ya Mipangomiji na Ramani za Upimaji na kupata upana wa barabara, kazi iliyofuata ni kufungua barabara. Barabara hizo zilifunguliwa  kwa kushirikiana na Manispaa ya Ubungo. Aidha uchongaji wa barabara umefuata vipimo vilivyoainishwa katika Michoro ya Mipangomiji na Ramani za Upimaji.

“Barabara zenye urefu wa kilomita 9.128 zimechongwa katika Mitaa ya Kilugule ‘A’, Kilungule ‘B’ na Mavurunza,” amesema Mlonda.

Katika urasimishaji huo, Mlonda aliainisha mafanikio ya mradi kama ifuatavyo: Kuwa na Michoro ya Mipangomiji na Ramani za Upimaji katika eneo la Kimara, kuboresha mazingira katika makazi, kuongeza huduma za jamii na miundombinu katika maeneo ambayo awali yalikuwa hayafikiki kwa gari sasa yanafikika na kuongeza usalama wa miliki ya ardhi kwa wananchi pamoja na  fursa ya kutumia ardhi kama mtaji na kupunguza umasikini.

Ameyataja mafanikio mengine kuwa kanzi data inajenga uwezo wa halmashauri kusimamia na kutoa huduma za ardhi kwa ufanisi, kuwa na maeneo yaliyopangwa, kupimwa na kumilikishwa, kupunguza au kuondoa kwa kiasi kikubwa migogoro ya ardhi na kuongeza wigo wa mapato ya serikali kupitia tozo mbalimbali za kodi ya ardhi.

Urasimishaji huu unatekelezwa kwa mkopo wa Benki ya Dunia ambapo viwanja 3000 vinatarajiwa kupimwa katika kila Halmashauri. Utekelezaji utatumia uzoefu uliopatikana wakati wa utekelezaji wa mradi katika Jiji la Dar es Salaam na Mwanza. Zoezi hili linalenga kuboresha hali ya mazingira katika maeneo yasiyopangwa na kuzuia ukuaji holela wa miji.

Aidha mradi huu utajenga uwezo wa halmashauri katika kutekeleza miradi na kuingiza urasimishaji makazi katika mipango kazi ya halmashauri.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi