Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Viwanda Vipya Kufungua Soko la Nafaka, Mazao Mchanganyiko
Oct 24, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Mwandishi wetu-MAELEZO

Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB), ina mkakati wa kufufua na kujenga viwanda vipya ili kuongeza thamani kwenye mazao ya kilimo kwa lengo la kuwa na soko zuri ndani na nje ya nchi.

Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Bodi hiyo Dkt. Anselm Moshi wakati akizungumza na wabahabari kuhusu utekelezaji na vipaumbele vya bodi hiyo kwa mwaka 2022/23.

“Tuna mikakati ya kumwezesha mkulima kuzalisha kwa tija kuongeza wingi wa mavuno ya mazao katika eneo dogo kwa kutumia kilimo cha mbinu za kisasa, pia tumeanza mkakati wa kupanua wigo wa masoko kwa kuwa na mbinu bunifu za kutangaza bidhaa zetu ikiwemo kutafuta masoko katika ukanda wa Afrika na ukanda wa nchi za mbali” amebainisha Dkt. Moshi.

Aidha, ameeleza kuwa kwa mwaka wa Fedha 2021/2022 Bodi imejenga kiwanda cha kukoboa mpunga eneo la Mkuyuni jijini Mwanza kwa thamani ya Shilingi bilioni 3.9, imekarabati miundombinu mbalimbali ya uhifadhi na gharama ya Shilingi milioni 967 na pia imejenga kiwanda cha kuchakata korosho mkoani Dar es Salaam kwa ajili ya kutengeneza siagi za korosho ambazo ni bidhaa inayotengenezwa na Bodi hiyo pekee hapa nchini na kuuza bidhaa hizo ndani na nje ya nchi.

“Tunawasaidia wakulima kupitia programu ya 'Kilimo Mkataba' ili waweze kuzalisha kwa tija, hii ni katika mikoa ya Kaskazini kwenye mikataba ya uzalishaji wa ngano, aidha wakulima wananufaika na kiwanda cha kuchakata ngano kilichopo Arusha kinachozalisha ngano tani 36,000 kwa mwaka, tunaendelea kuhamasisha uzalishaji zaidi wa kilimo cha ngano ili tupunguze kiwango cha kuagiza ngano kutoka nje” amefafanua Dkt. Moshi.

Katika hatua nyingine Dkt. Moshi amebainisha maeneo ya kipaumbele kwa mwaka wa Fedha 2022/2023 ikiwemo mpango wa kuzalisha ngano hapa nchini tani milioni moja ndani ya miaka mitano kuanzia sasa na kuongeza uwezo wa kuhifadhi mazao kutoka tani 122,800 hadi tani 600,000 ndani ya miaka mitano.

Mbali na hayo Bodi hiyo inaboresha matumizi ya teknolojia na TEHAMA kwa kuwajengea uwezo wafanyakazi wao kiutendaji ili kuwa na tija na kuweza kuingiza faida kupitia biashara wanayoifanya ndani na nje ya nchi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi