Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Vipaumbele 2023/24 Kuifanya BMH Kuendeleza Ubingwa Bobezi
Aug 01, 2023
Vipaumbele 2023/24 Kuifanya BMH Kuendeleza Ubingwa Bobezi
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Dkt. Alphonce Chandika akizungumza na Waandishi wa Habari leo jijini Dodoma katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO kuhusu utekelezaji wa Hospitali hiyo na vipaumbele vyake kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Dkt. Alphonce Chandika amesema kuwa vipaumbele vya bajeti ya Mwaka wa Fedha 2023/24 vilivyowekwa na Taasisi hiyo vimelenga kuifanya hospitali hiyo kuendelea kuwa hospitali ya Ubingwa Bobezi (Super Specialized) ambapo mpaka sasa ina uwezo wa kuhudumia wananchi zaidi ya milioni 10 hasa mikoa ya Dodoma, Iringa, Singida, Manyara na baadhi ya Maeneo ya Mikoa ya Morogoro na Tabora pia, nje ya mipaka ya Tanzania.

Dkt. Chandika ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO kuhusu utekelezaji wa Hospitali hiyo na vipaumbele vyake kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

“Kwa mwaka huu wa fedha, tumetengewa jumla ya shilingi 64,527,012,327/= ambapo kati yake, jumla ya shilingi 18,620,000,000/= zinakwenda kwenye miradi ya maendeleo ili kuendelea kuwapunguzia wananchi adha ya kusafiri mbali kupata matibabu, mradi mmoja wapo ni kuendeleza ujenzi wa jengo la Saratani ambalo mpaka sasa umefikia asilimia 27”, amesema Dkt. Chandika.

Miradi mingine ni kuanza ujenzi wa jengo la matibabu ya moyo na kifua kwa watoto na watu wazima pamoja na kuongeza vyumba vya upasuaji ili kukidhi hitaji la wagonjwa, kujenga kituo cha upandikizaji wa figo chenye vyumba vya upasuaji kwa anayechangia figo na anayepokea, Maabara ya kuchukulia sampuli za wagonjwa, chumba cha wagonjwa mahututi pamoja na duka la dawa na vyumba vya madaktari, kuimarisha Chuo cha Tiba na Sayansi Shirikishi kwa kujenga mabweni na maabara maalum ya mafunzo kwa vitendo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi