Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Viongozi wa Dini Wataka Watoa Huduma za Usafiri Majini Kuzingatia Kanuni
Sep 25, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na Tiganya Vincent - RS Tabora

Viongozi wa Dini Mkoani Tabora wamewataka watumiaji wa vyombo vya usafiri majini kuzingatia taratibu na  sheria zinazoongoza usafiri huo ili kuepusha maafa ambayo yanaweza kuzuilika.

Wametoa kauli hiyo wakati wa maombi maalumu ya kuwaombea marehemu ya ajali ya MV Nyerere iliyotokea wiki iliyopita (tarehe 20 Septemba 2018)  katika Kisiwa cha Ukerewe na kusababisha vifo vya watu 227.

Sheikh ya Mkoa wa Tabora Ibrahim Mavumbi alisema Watendaji wa MV Nyerere hawakuchukua tahadhari jambo ambalo limesababisha familia nyingi kuingia katika majonzi ambayo yamepelekea  baadhi yao kubaki wajane, yatima na wagane.

Alisema wasafirishaji ni vema wakazingatia makatazo ambayo yanasimamia usafiri huo ili kutosababisha maafa mengine makubwa kwa Taifa kama ambayo yametokea kwa sababu ya uzembe.

Naye Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Tabora, Elias Chakupewa alisema ajali hiyo imeacha machungu kwa watanzania kwa kupoteza wananchi wengi kwa wakati mmoja wakiwemo watoto wadogo ambao ndio wangekuja kuwa nguvu kazi ya Taifa siku za baadae.

Alisema pamoja na kuwa vifo ni mpango wa Mungu lakini ajali hiyo inaonyesha jinsi gani viongozi wa Meli hiyo na Watendaji wengine hawakuchukua hatua na kuamua kuzidisha abira na mizigo jambo lilichangia maafa hayo.

Chakupewa alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dokta John Pombe Magufuli kwa hatua za haraka alizochukua  mara baada ya kutokea ajali hiyo ikiwa ni pamoja na kumtuma Waziri Mkuu kwenda kwenye eneo la ajali na Mawaziri mengine na kuwachukulia hatua baadhi ya watendaji  ikiwemo kuvunja Bodi ya TEMESA na SUMATRA.

Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri alisema hakuna haja ya kutofautiana kwa sababu ya msiba uliotokea wa kuzama kwa meli ya MV Nyerere na kuongeza kuwa ajali hiyo isiwatenganishe na Mungu.

Aliwataka watu wote waliopatwa na msiba huo mkubwa na Watanzania kumtanguliza Mungu katika wakati huu mgumu.

Maombi hayo yaliandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ikiwa ni siku ya mwisho ya maombolezo ya kitaifa kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea Watanzania waliopoteza maisha kutoka na kuzama kwa MV Nyerere.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi