Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Vijana 240 Kuwezeshwa Kujiajiri Sekta ya Mifugo
Aug 14, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Mbaraka Kambona

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amesema kuanzia mwaka huu wa fedha 2022/23 Wizara kupitia Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) na Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (LITA) imeanzisha vituo atamizi nane (8) ambavyo vitahusisha vijana 240 waliohitimu taaluma za mifugo kwa ajili ya unenepeshaji mifugo katika vituo vilivyopo katika Mikoa ya Tanga, Kagera, Songwe na Mwanza.

Waziri Ndaki alisema hayo jijini Dodoma mwishoni mwa wiki katika taarifa yake kwa umma kuhusu utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa kwenye kilele cha maadhimisho ya sherehe za Wakulima (NaneNane) yaliyofanyika jijini Mbeya Agosti 8, 2022.

"Nimeziagiza taasisi hizo kuanza ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya unenepeshaji wa mifugo mara moja na kukamilisha taratibu za kuwapatia vijana", alisema Ndaki.

Alisema kuwa ili kufanikisha hilo, Wizara itashirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo wahitimu wajasirimali wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wanaofahamika kama SUGECO, Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), Benki ya CRDB, Viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo nchini, Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Taasisi ya Dhamana ya Uwezeshaji Kilimo (PASS) na NARCO.

Aliongeza kuwa baada ya kupitia mikataba na mipango ya kibiashara kwa kila mwekezaji katika vitalu vya NARCO watatenga vitalu vya unenepeshaji wa mifugo kwa ajili ya kuwapangisha vijana hao watakaohitimu katika vituo hivyo atamizi.

Kuhusu tathmini ya upangishaji wa vitalu vya NARCO, Mhe. Ndaki alisema kuwa Wizara imeunda timu ya Wataalam kutoka Serikalini na taasisi mbalimbali za sekta binafsi kufanya tathmini ya kina ya Utendaji na changamoto zinazoikabili Kampuni hiyo ili waweze kuishauri vizuri Serikali.

Aliongeza kwa kusema kuwa NARCO inafanya mapitio ya mikataba na mipango ya biashara kwa kila mwekezaji kulingana na mikataba yao ili kubaini hali halisi ya uwekezaji.

Ili uwekezaji wenye tija katika Ranchi za NARCO uweze kufanyika kikamilifu, Waziri Ndaki alisema NARCO imeainisha na kutenga vitalu vitano (5) vyenye ukubwa wa takriban hekta 32,500 ili kuvutia wawekezaji mahiri na wenye mitaji kutoka ndani na nje ya nchi.

Agosti 8, 2022 akiwa jijini Mbeya, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan aliitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ili kuwawezesha vijana kujiajiri katika sekta ya mifugo na kufanya maboresho makubwa ya utendaji wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO).

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi