Bodi ya Mkonge Tanzania kuhakikisha kuwa uzalishaji unaongezeka hadi kufikia tani 120,000 ifikapo mwaka 2025/2026 kutokana na hatua za Serikali kuliingiza zao la mkonge kwenye orodha ya mazao ya kimkakati.
Akieleza kwa Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio ya Bodi hiyo leo jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Bodi hiyo Bw. Saady Kambona amesema kuongezeka kwa uzalishaji kunatokana na kugundulika kwa matumizi mapya ya Mkonge na uzalishaji wa bidhaa mpya zitokanazo na mkonge kama vile vifaa vya ujenzi matofali, mbao, mabati, vigae, sukari ya mkonge, pombe ya mkonge, karatasi maalum, mbolea, chakula cha mifugo , urembo na bodi za magari.
“Napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru na kumpongeza kwa dhati kabisa Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua za kimageuzi alizochukua na anazoendelea kuchukua katika kuleta mageuzi ya kweli kwenye zao la Mkonge na Sekta ya kilimo kwa ujumla”, alisisitiza Kambona
Akieleza mafanikio ya Bodi, Bw. Kambaona amesema kuwa kuongezeka kwa uzalishaji wa Mkonge kutoka tani 36,379 kwa mwaka yaani mwaka 2020 hadi kufikia tani 48,351.49 mwaka 2022.
Kuongezeka kwa fedha za maendeleo kutoka shilingi milioni 100 mwaka 2019/2020 hadi kufikia shilingi bilioni mbili mwaka 2022/2023 na kuipatia Bodi hiyo vyombo vya usafiri ili kurahisisha utendaji kazi wa taasisi ambapo kwenye Bajeti ya 2021/2022 wamepatiwa magari matatu na pikipiki tatu.
Aidha, Kambona amesema kuwa fedha za makusanyo ya ndani zimeongezeka kutoka shilingi 0.00 mwaka 2019/2020 hadi shilingi milioni 507 mwaka 2022/2023 na pia kukukusanya na kusambaza miche 6,991,200 ya mbegu za Mkonge bure kwa wakulima wadogo katika Wilaya 16 za Korogwe,Muheza, Tanga, Mkinga, Handeni, Kilindi, Rorya, Bunda, Butiama, bariadi, Bagamoyo(Chalinze), Kisarawe, Mkuranga, Manyoni(Itigi), Singida Vijijini na Mkalama.
Mwaka 2020 Bodi ilisajili wakulima wadogo 6,887 na mwaka 2022 idadi ya wakulima wadogo waliosajiliwa ni 8,972. Aidha, kushusha riba kwenye mabenki ya biashara kwa mikopo inayoelekezwa kwenye kilimo na hivyo kuleta unafuu mkubwa kwa wakulima ambapo riba kwa mikopo ya kilimo sasa kwa ujumla haizidi asilimia 9%.