Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Uwekezaji wenye Dosari Mbioni Kusitishwa Ziwa Babati
Aug 11, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki na Waziri wa Nchi-Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhe. Selemani Jafo wanakusudia kusitisha uwekezaji uliofanywa katika Ziwa Babati na kampuni ya watu wa China ya XIN SI LIU mara baada ya kuonekana kuna dosari kadhaa zilizoainishwa na mamlaka zilizo chini ya Wizara hizo.

Mawaziri hao walibainisha hilo jana (10.08.2022) mkoani Manyara wakati wa mkutano wa majumuisho mara baada ya kwenda kutembelea eneo linalokusudiwa kuwekwa mradi huo na kupokea taarifa kutoka kwenye mamlaka zilizokuwa zikifanya tathmini ya uwekezaji huo.

Akizungumza juu ya aina ya uwekezaji uliotarajiwa kufanyika katika eneo hilo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki alisema kuwa kwa mujibu wa taarifa waliyopokea na hali waliyoiona, ufugaji wa samaki kwenye vizimba kwenye eneo hilo la Ziwa hauwezi kuwa na matokeo chanya kwa Mwekezaji na utasababisha mgogoro baina ya wananchi na Serikali, hivyo amemshauri Mwekezaji huyo kuangalia eneo jingine ambalo anaweza kufanya uwekezaji wenye faida kwake na tija kwa Taifa kwa ujumla.

“Kwenye rasilimali yoyote ni lazima yaangaliwe maslahi ya pande zote mbili ambayo ni upande wa Mwekezaji na upande wa wanufaika wa uwekezaji huo au wadau wanazunguka eneo la uwekezaji na kazi yetu kama Serikali ni kupima na kuangalia uzito uko wapi zaidi”, aliongeza Ndaki

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi-Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. Selemani Jafo alisema kuwa, taarifa iliyotolewa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) imeainisha athari za kimazingira zitakazotokea kwa upande wa Ziwa Babati kutokana na uwekezaji huo ambapo aliwataka wataalam kuendelea kuwashauri wawekezaji juu ya usahihi na usalama wa maeneo wanayokusudia kuwekeza.

Awali akipendekeza kusitishwa kwa uwekezaji huo, Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini, Mhe. Pauline Gekul alisema kuwa uwekezaji huo utaibua migogoro kwa wananchi wa Wilaya hiyo hasa kutokana na Ziwa hilo kutegemewa na zaidi ya wavuvi 1,000 kuendesha maisha yao.

Kampuni ya China ya XIN SI LU ilikuwa inakusudia kufanya uwekezaji wa ufugaji wa samaki kwenye vizimba katikati ya ziwa Babati ambapo ilitarajia kuchukua eneo la ukubwa wa hekari tatu kwa ajili ya shughuli hiyo jambo ambalo limeonekana kuwa na athari ya mazingira na kiuchumi kwa wananchi wanaonufaika na ziwa hilo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi