Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Uwekezaji Bandari ya Dar es Salaam Wazaa Matunda
Dec 05, 2023
Uwekezaji Bandari ya Dar es Salaam Wazaa Matunda
Naibu Waziri wa Wizara ya Uchukuzi, David Kihenzile akizungumza na wadau wa usafirishaji (hawapo pichani) wakati wa hafla ya upokeaji wa meli ya makasha ya Kampuni ya Huduma za Meli ya Emirates iliyowasili kwa mara ya kwanza kutokea nchini China. Hafla hiyo ilifanyika katika bandari ya Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu

Serikali imesema kukamilika kwa sehemu ya miradi ya maboresho ya miundombinu ya Bandari ya Dar es Salaam kumeanza kuleta matokeo chanya kwani kupitia maboresho hayo kumekuwa na ongezeko la idadi ya shehena inayohudumiwa kwa mwezi kutoka makasha elfu themanini (80) hadi kufikia laki moja kwa mwezi.

 

Akizungumza wakati wa halfa ya kupokea meli ya makasha ya Kampuni ya Emirates Shipping Lines (ESL) iliyoanza rasmi kufanya safari za moja kwa moja kutoka nchini China kuja Tanzania kupitia bandari ya Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Wizara ya Uchukuzi, David Kihenzile amesema Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ili kurahisisha usafirishaji na uchukuzi nchini. 

 

“Ujio wa meli hizi zinazofanya safari za moja kwa moja kutoka nchini China hadi Tanzania ni mwendelezo wa matokeo yanayojionyesha baada ya kukamilika kwa maboresho yanayofanywa na Serikali kwenye miundombonu ya bandari nchini, pongezi hizi zinatakiwa kwenda moja kwa moja kwa uongozi shupavu wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu”, amesema Naibu Waziri Kihenzile.

Naibu Waziri wa Wizara ya Uchukuzi, David Kihenzile (kulia) akimsikiliza Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Mrisho Mrisho kuhusu utendaji wa bandari hiyo wakati wa hafla ya upokeaji wa meli ya makasha ya Kampuni ya Huduma za Meli ya Emirates iliyowasili kwa mara ya kwanza kutokea nchini China. Hafla hiyo ilifanyika katika bandari ya Dar es Salaam jijini humo.

Naibu Waziri Kihenzile amesema pamoja na ongezeko hilo la shehena, ujio wa meli hizo utapunguza gharama za usafirishaji kwani mzigo utapakiwa nchini China na kuja moja kwa moja nchini Tanzania hivyo kupunguza gharama za usafirishaji wa shehena hususani makasha. 

 

Aidha, Naibu Waziri Kihenzile amechukua fursa hiyo kuielekeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuhakikisha meli zote zinazotoa hudhuma kupitia bandari nchini zinapewa huduma stahiki na zenye viwango.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Mrisho Mrisho amesema baada ya maboresho makubwa yaliyohusisha ujenzi wa gati na uongezaji wa kina katika lango la kuingilia bandarini kumeiwezesha bandari kuongeza idadi ya mizigo na magari inayohudumiwa kwa wakati mmoja.

 

Mkurugenzi Mrisho amemuhakikshia Naibu Waziri Kihenzile kuwa kwa sasa TPA imejipanga kuhakikisha kuwa inatumia vizuri mitambo iliyonayo kutoa huduma kwa uharaka na ufanisi hususani katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka.

 

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Huduma za Meli ya Emirates (ESL) Kanda ya Afrika Mashariki, Nahodha Nithin Nath amesema kuanza kutoa huduma za kusafirisha mizigo moja kwa moja kutoka China hadi Tanzania kunatarajiwa kupunguza muda wa safari na usafirishaji kutoka siku 45 hadi siku 22 na hivyo kufanya bei za bidhaa kushuka.

Nahodha Nath amesema ESL imeweka mikakati ya kuhakikisha inaanzisha safari za kusafirisha makasha ya mizigo kutoka China kwenda bandari za Tanga, Mtwara na Zanzibar.

 

Meli ya Kampuni ya ESL imefanya safari yake kwa mara ya kwanza kutoka nchini China kuja Tanzania na kwa safari hiyo itaweza kushusha na kupakia makasha takribani 600 ambapo kazi hiyo inatarajiwa kufanywa ndani ya saa zisizozidi 48.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi