Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema Watanzania wana kila sababu ya kulinda utamaduni na utu wao na katu wasiudhalilishe dhidi ya utamaduni wa kigeni.
Dkt. Biteko amesema hayo tarehe 29 Februari, 2024 wakati akizungumza katika mkutano wa mwaka wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa uliofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa Mfuko huo.
“Kupitia kazi za sanaa lazima tuoneshe kuupenda utamaduni wetu na kuuishi na tunataka utamaduni huo uende mpaka nje ya mipaka ya nchi, kwani Taifa lisilo na utamaduni ni Taifa mfu hivyo tuuenzi utamaduni wetu ambao ni mzuri.” Amesema Dkt. Biteko
Dkt. Biteko amewasifu Wasanii nchini kwa kukataa kupuuza utamaduni wa Taifa na kuamua kwa pamoja kuupa heshima utamaduni huo kupitia kazi zao za sanaa.
Amesema kuwa, Wasanii wanao wajibu mkubwa wa kulifanya Taifa kuwa hai, kuliondoa kwenye wimbi la kupotea duniani na kuwafanya Watanzania waone lugha yao, tamamduni zao na desturi za Tanzania zinapaswa kuheshimiwa na kila mtu.
Ameongeza kuwa, kwa miaka mingi kazi ya Sanaa ilikuwa ni kuelimisha na kuburudisha lakini sasa imepanuka na imekuwa ni nyenzo ya kutengeneza ajira na ndio maana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan aliamua kuufufua mfuko huo ambao ulianzishwa mwaka 1992 na ambao ulikuwa ukisuasua lakini sasa umeimarika.
Dkt. Biteko amepongeza Wasanii wote ambao wamekuwa wakizingatia vigezo na mashati ya kukopa na kurejesha mikopo kwa wakati na hivyo kuwataka Wasanii kuhimizana juu ya umuhimu wa kukopa na kurejesha mikopo ili iweze kuwanufaisha wengine.
Amesema pamoja na ukweli kwamba sekta ya utamaduni na sanaa inaongoza kwa ukuaji kati ya sekta zote nchini ikikua kwa asilimia 19 lakini bado mchango wake kwa pato la Taifa ni duni kwani inachangia asilimia 0.3 na hii ikimaanisha kuwa Sekta inakua lakini haichangii zaidi.
Ameiagiza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuweka mazingira mazuri kwa Wasanii ili kukuza sekta ya utamaduni na sanaa sambamba na ukuaji wa uchumi.
Vilevile, Dkt. Biteko ameitaka Wizara kuwa kiungo cha wasanii na Serikali hasa katika kazi ambazo wananchi wanapaswa kupata ujumbe au kuhamasishwa akitolea mfano matumizi ya nishati safi ya kupikia, afya na mazingira na kwamba Wasanii hao wanapaswa kupata mapato stahiki.
Aidha, pamoja na kuzipongeza Benki ya NBC na CRDB kwa kuwa wadhamini na wakopeshaji kwenye suala hilo ametaka Benki zinazotoa mikopo kwa wasanii hao kulegeza masharti ili wasanii wengi zaidi waweze kupata mikopo na kuweza kuirejesha kwa wakati.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amewataka Wasanii kutumia kazi zao za Sanaa kuhamasisha wananchi kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka huu ili wananchi hao waweze kujitokeza kwa wingi na kuchagua viongozi wanaopenda maendeleo na kuunganisha wananchi.
Kwa upande wake, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake na upendo wake kwa Wasanii nchini ndio maana ameufufua mfuko huo na kuweka fedha ambazo zinawasaidia wasanii katika kuanzisha, kuboresha na kupanua shughuli zao za Sanaa.
Amesema kuwa, pamoja na faida mbalimbali za mkopo huo, bado kuna changamoto kama vile wakopaji kutorejesha mikopo kwa wakati na mfuko kuwa na chanzo kidogo cha fedha ambapo Wizara inachukua hatua mbalimbali kushughulikia changamoto hizo.
Amesema kuwa, katika Mfuko huo, itaanziswa sehemu ya kutoa mafunzo maalum kwa wasanii wachanga ya kuwanoa na kuwawezesha kuunda taasisi ambayo itakua na itakubalika kwenye benki ili kupata mikopo.
Ameongeza kuwa, Wizara hiyo inaangalia sekta ya Sanaa na Utamaduni kama chanzo cha ajira na uchumi hivyo ameomba wadau mbalimbali kuunga mkono juhudi hizo za Serikali.
Awali, Mwenyekiti wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa, Abdulmajid Nsekela alisema kuwa, mfuko huo unatoa huduma kuu tatu ambazo ni mikopo ya masharti nafuu kwa walengwa katika sekta, kuwajengea uwezo wasanii kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo ujasiriamali, urasimishaji, nidhamu
ya biashara na kuwapa nafasi ya kuona fursa mpya zilizopo kwenye Sekta.
Ameongeza kuwa, katika siku za usoni mfuko unalenga kutoa ruzuku ili kuwawezesha wajasirimali katika sekta hiyo.
Viongozi waliohudhuria Mkutano huo ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato, Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma.