Jovina Bujulu.
Hivi karibuni Serikali itasambaza vifuko maalum 500 kwa ajili ya kuwasaidia wakina mama wajawazito kujifungua salama.
Ahadi hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Dk Khamis Kigwangalla alipokuwa akijibu maswali bungeni kuhusu huduma zinazotolewa na hospitali na vituo vya afya hapa nchini.
Hatua hii ya kusambaza vifuko hivyo itakuwa ni mkombozi kwa wajawazito katika kupunguza au kuondoa kabisa matatizo yanayowakuta wakati wakienda katika vituo vya afya kwa ajili ya kujifungua.
Takwimu zilizotolewa na Mratibu wa Taifa wa Chama cha Wakunga Tanzania (TAMA), Bi. Martha Rimoy zinaonyesha ongezeko la vifo vya wakina mama wajawazito wakati wa kujifungua kuwa ni kutoka 454 hadi 556 kwa kila vizazi hai 100,000 kwa kipindi cha mwaka 2015-16.
Vifo hivyo ni sawa na wakina mama 1,255 kila mwezi, 42 kila siku na wawili kila saa moja. Ongezeko hilo ni kubwa sana na Taifa linapoteza nguvu kazi ya wakina mama hao ambao wangeweza kukuza uchumi wa Taifa. Takwimu hizo ni kigezo kimojawapo cha kupima umaskini wa nchi.
Mratibu huyo alibainisha sababu mojawapo inayochangia ongezeko hilo kuwa ni pamoja na upungufu wa vifaa tiba , ufinyu wa bajeti ya afya na upungufu wa wakunga wenye ujuzi stahiki.
Suala la afya ya mama na mtoto ni ajenda muhimu ya dunia katika malengo ya maendeleo endelevu, hivyo suala la kusambaza vifuko hivyo litapunguza au hata kumaliza kabisa tatizo la vifo vitokanavyo na uzazi .
Aidha , Wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi , ni budi kusimamia kwa dhati usambazaji na matumizi sahihi ya vifuko hivyo ili kuleta mabadiliko chanya katika suala la vifo vitokanavyo na uzazi.
Pia wakina mama wajawazito ni wakati wao wa kujitokeza kuhudhuria kliniki badala ya kujifungulia nyumbani il wafaidike na huduma hii ambayo inatolewa bure.
Dk Kigwangala alisisitiza kuwa Serikali haijawahi kuweka tozo au gharama katika vifaa tiba vya uzazi, vifaa hivyo hutolewa bure katika vituo vyote na ngazi zote zinazotoa huduma za afya.
Aliongeza kuwa azma ya Serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha kuwa wajawazito wanapata huduma nzuri na kupunguza vifo vya mama na mtoto vitokanavyo na uzazi, hii ikiwa ni utekelezaji wa Sera ya Afya ya mwaka 2007.
Kila mwaka jumla ya wanawake wajawazito 1,900,000 hujifungua, ambapo wengi wao wanakabiliwa na changamoto za vifo vitokanavyo na uzazi. Kusambazwa kwa vifuko hivyo kutaongeza idadi ya wakinamama wanaojifungulia katika vituo vya afya na kuongeza mahudhurio ya wajawazito kliniki ili kufuatilia mwenendo wa afya zao.