Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Ummy Mwalimu Atahadharisha Tishio la UVIKO-19 Wimbi la Tano
Jun 02, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Ataka wengi kuchanja, kujikinga.

Na Grace Semfuko MAELEZO

Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu amesema Tanzania inaendelea na mikakati ya kukinga kusambaa kwa maambukizi ya ugonjwa wa UVIKO- 19 na ndio maana Serikali inafanya kila jitihada za kukabiliana na ugonjwa huo.

Amesema tishio la wimbi la tano la maambukizi ya ugonjwa huo lipo, na hivyo Tanzania inaungana na nchi nyingi zingine Duniani kupambana na kuhakikisha hakuna maambukizi mapya.

Ameyasema hayo leo Juni 02, 2022 wakati akizindua Mkakati wa Dunia wa kuhamasisha zoezi la kuchanja ili kuepukana na ugonjwa wa UVIKO-19 (Global Vax Initiatives) inayodhaminiwa na Serikali ya Watu wa Marekani ambapo imetajwa kuwa, Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri katika chanjo.

"Nimepewa na Rais Samia Suluhu Hassan kusimamia afya za Watanzania, niseme wazi kwamba bado tunao ugonjwa wa Korona nchini kwetu, ugonjwa upo lakini tunaowaona wanaoteswa na ugonjwa huu ni wale ambao hawajachanja, kwa hiyo kwa sababu ugonjwa wa UVIKO 19 bado upo, na kwa sababu tupo katika tishio la kupata wimbi la tano la ugonjwa huu, ndio maana leo tunazindua mpango huu wa Global Vax ili kuweza kuwatayarisha watanzania kupambana na wimbi linalokuja la UVIKO 19, tumepita katika mawimbi manne ya ugonjwa huu, na kama wizara ya afya tunaendelea kufuatilia kwa karibu sana ugonjwa huu.” Amesema Mhe. Mwalimu.

Katika hotuba yake, Balozi wa Marekani Nchini Tanzania, Dkt Donald Wright ameipongeza Tanzania kwa kuchaguliwa kuwa miongoni mwa nchi chache zilizopokea ongezeko la rasilimali hizi kupitia Mpango wa Global VAX na kusema kuwa Marekani imejitolea kuisaidia Tanzania katika mapambano yake dhidi ya UVIKO-19.

“Tunapokabiliana na aina tofauti za virusi vya UVIKO-19 vilivyoathiri kila nchi duniani kote, tunakumbushwa kwamba hakuna hata moja wetu aliye salama hadi tuwe salama wote. Ni jukumu letu kuhakikisha wote tunapata chanjo ya UVIKO-19,” alisema Balozi Wright.

Kwa upande wake Kaimu Mwakilishi Mkazi wa wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), Dkt. Zabulon Yoti amesema chanjo ya UVIKO-19 ni muhimu kwa kuwa inaokoa maisha ya watu na kuipongeza Tazania kuunga mkono juhudi za shirika hilo katika mapambano ya magonjwa mbalimbali.

“Nataka kuwahakikishiwa watu wa Tanzania kuwa chanjo inafanya kazi, chanjo inaokoa maisha, kupitia chanjo magonjwa mengi yanatoweka hapa nchini, leo nchi nyingi duniani zinachukua tahadhari kwa kupata chanjo ikiwepo ya UVIKO-19 na kwa kufanya hivi tunafungua uchumi wa Dunia, biashara zinakwenda vizuri, nguvu zetu katika kukabiliana na ugonjwa huu tunashirikiana kwa pamoja na wadau na nawashukuru sana kwa ushirikiano huu,” amesema Dkt. Yoti.

Chanjo ya UVIKO-19 ilizinduliwa kwa mara ya kwanza nchini na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan Julai 28, 2021, ambapo mpaka sasa watu Milioni 4.6 ikiwa ni sawa na asilimia 15.2 ya watanzania wenye umri wa miaka 18 na kuendelea wamepatiwa chanjo hiyo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi