Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Ukatili Wa Kingono Bado Changamoto Kwa Wasichana Hapa Nchini
Jun 15, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na: Anthony Ishengoma - Maendeleo ya Jamii

Wasichana Nchini Tanzania wanakumbana na changamoto mbalimbali  katika  makuzi yao ikiwemo ukatili wa kingono na mimba za utotoni .

Akiongea na vyombo vya habari mjini Dodoma leo wakati wa Kongamano la maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika,Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Hamis Kigwangala amesema takwimu zinaonesha kuwa asilimia 51.4 ya idadi ya watoto nchini ni wasichana.

”Mtoto wa kike 1 kati ya watoto 3 na mtoto wa kiume 1 kati ya 7 wanakumbana na ukatili wa kingono kabla ya kufikia umri wa miaka 18,” alisema Kigwangala.

Aidha Dkt. Kigwangala amesema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa uwiano wa wasichana na wavulana katika elimu ya msingi na sekondari ni uwiano wa moja kwa moja (1:1), ingawa idadi ya wasichana hupungua kutokana na changamoto wanazokutana nazo ikiwa ni pamoja na mimba na ndoa za utotoni.

”Kwa mujibu wa takwimu za elimu kwa Mwaka 2012 hadi 2016  idadi ya watoto wa kike walioacha shule kutokana na  kupata ujauzito  ni 610 (mwaka 2011), 2,433 (mwaka 2012), 247 (mwaka 2013), 265 (mwaka 2014) na 251 (mwaka 2015). Serikali inaendelea kukabiliana na changamoto hizi ili kuhakikisha wanafunzi wa kike wanapata elimu hadi kufikia ngazi ya vyuo alisema Dkt. Kigwangala’’.

Ameeleza madhumuni ya kuadhimisha siku hiyo kuwa ni  kutoa fursa kwa wazazi, walezi na wadau wote wa haki za mtoto kutafakari changamoto zinazowakabili kama vile ukatili katika Bara letu la Afrika kwa lengo la kuzipatia ufumbuzi.

Maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika hapa nchini hutumika  kutathmini changamoto zinazowakabili watoto katika upatikanaji wa haki, malezi, elimu, afya na ulinzi kwa lengo la kuboresha huduma hizo ili ziweze kumfikia kila mtoto nchini.

Aidha amesema siku hiyo inatumika kuwakumbusha na kuwahimiza wazazi, walezi na jamii kwa ujumla  kuzingatia jukumu lao la msingi la utoaji haki na huduma za ustawi wa mtoto bila ubaguzi wowote. Siku hii hutumika kufanya ushawishi kwa wadau kuwekeza katika maeneo ya malezi, afya, elimu, ulinzi kwa lengo la kuunga mkono jitihada za Serikali za kumwendeleza mtoto.

Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yametokana na Azimio lililopitishwa na iliyokuwa Jumuiya ya Nchi Huru za Umoja wa Afrika (OAU) kwa ajili ya kukumbuka mauaji ya watoto wa shule  yaliyofanyika  katika kitongoji cha Soweto, nchini Afrika ya Kusini tarehe 16 Juni 1976.

Aidha Katika tukio hilo la kusikitisha, inakadiriwa kuwa takribani watoto 700 waliuawa kikatili wakiwa kwenye harakati za kupinga mifumo ya elimu ya kibaguzi iliyokuwa inataolewa na serikali ya makaburu.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi