Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Ujenzi wa Majengo ya Ghorofa Mtumba Washika Kasi
Aug 17, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Katibu wa Kikosi Kazi cha Taifa cha kuratibu Serikali kuhamia Dodoma na ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba, Meshack Bandawe amekutana na Wakurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara zote ili kujadili  maandalizi na utekelezaji wa ujenzi wa ofisi za ghorofa za Wizara zitakazojengwa awamu ya pili katika Mji wa Serikali Dodoma.

Kikao hicho kinafuatia maelekezo ya Mhe. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyezitaka Wizara kuanza taratibu za ujenzi wa ofisi za awamu ya pili baada ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kutoa kiasi cha shilingi bilioni 300 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa miundo mbinu na majengo ya ghorofa yatakayotumiwa na wizara mbalimbali katika mji wa Serikali Mtumba.

“Kwa kuwa Wakurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ndiyo timu ya ufundi ya usimamizi wa ujenzi na wasaidizi wa makatibu wakuu ni vyema tukajipanga kikamilifu ili kutekeleza ujenzi kwa tija, ufanisi, ubora, muda, kanuni, taratibu  na kwa mujibu wa bajeti iliyotengwa na Serikali”, alisema Bandawe katika kikao hicho.

Kwa mujibu wa bwana Bandawe, kikao hicho pia ni maandalizi ya vikao vitakavyofuata vya Makatibu Wakuu na Mawaziri kwa ajili ya kupokea maagizo na maelekezo ya Serikali katika kutekeleza shughuli za ujenzi kwa ufanisi.

Awamu ya kwanza ya ujenzi wa Mji wa Serikali ilikamilika Aprili, 2019 na kuwezesha Wizara na taasisi mbalimbali za Serikali kuhamishia ofisi zake mkoani Dodoma ambapo ujenzi wa awamu ya pili ya mji huo unatarajiwa kuanza muda wowote kuanza sasa baada ya Serikali kutoa pesa kwa ajili ya kuendeleza ujenzi huo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi