Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), Lazaro Kilahala, mwishoni mwa wiki hii ametembelea Yadi ya Songoro iliyopo wilayani Ilemela mkoani Mwanza kukagua maendeleo ya ujenzi wa vivuko vipya vinne na ukarabati wa vivuko unaoendelea mkoani humo.
Vivuko hivyo vinne vinavyojengwa ni pamoja na kivuko kitakachokwenda kutoa huduma kati ya Ijinga na Kahangala wilayani Magu, kivuko kitakachokwenda kutoa huduma kati ya Bwiro na Bukondo wilayani Ukerewe, kivuko kitakachokwenda kutoa huduma kati ya Kisorya na Rugezi wilayani Ukerewe pamoja na kivuko kitakachokwenda kutoa huduma kati ya Nyakaliro na Kome wilayani Sengerema, vyote vikiwa mkoani Mwanza.
Akizungumza mara baada ya kukagua vivuko hivyo, Mtendaji Mkuu amesema ujenzi wa vivuko hivyo unakwenda vizuri na kwa wastani vimefikia asilimia sitini (60%) ya ujenzi wake. Mtendaji Mkuu amesema vifaa karibia vyote ambavyo vilikuwa vinasubiriwa kwa ajili ya kufungwa kwenye vivuko hivyo vipya tayari vimekwishawasili bandarini na tayari mkandarasi wa ujenzi wa vivuko hivyo amekwishalipwa malipo ya awali na taratibu za kuvitoa vifaa hivyo bandarini zinaendelea.
‘’Kama ambavyo tumejionea ujenzi unakwenda vizuri, hivi ni vivuko vipya kabisa vinavyojengwa na Serikali yetu chini ya Rais wetu, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, ni Imani yetu kwamba kati ya mwezi huu wa nane mpaka mwezi wa kumi na mbili hatua kubwa sana ya ujenzi itakuwa imefanyika katika vivuko hivi,’’ amesema Kilahala.
Vilevile, Mtendaji Mkuu ambaye aliambatana na Meneja wa Vivuko Kanda ya Ziwa na Magharibi Mhandisi Vitalis Bilauri, amekagua pia maendeleo ya ukarabati wa vivuko unaoendelea katika Yadi hiyo ambapo amesema tayari kivuko cha MV. MISUNGWI ambacho kilikuwa kinakarabatiwa na Mkandarasi Songoro kimerejea kutoa huduma katika eneo la Kigongo na Busisi.
Kilahala ameongeza kuwa kivuko cha MV. UJENZI nacho kimekamilika na tayari kimerudishwa Kisorya Rugezi kuendelea kutoa huduma, kivuko cha MV. MUSOMA tayari kimefanyiwa majaribio na kimekamilika na tayari kimerejeshwa eneo la Musoma Kinesi kuendelea kutoa huduma, aidha ameongeza kuwa kivuko cha MV. MARA kiko katika hatua za mwisho za ukarabati wake sambamba na kivuko cha MV. Nyerere, ameongeza Mtendaji Mkuu huku akitoa shukrani kwa Serikali kwa kuendelea kufadhili miradi hiyo.
“Kwa ujumla tunaishukuru sana Serikali yetu kwa mkazo mkubwa ambao inaweka kwenye kuhakikisha vivuko vyetu vinafanyiwa ukarabati na vingine vipya vinajengwa kwa wakati ili viweze kuendelea kuboresha huduma kwa wananchi wetu, tunamshukuru sana Rais wetu Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, lakini pia tunaishukuru Wizara yetu ya Ujenzi na Uchukuzi chini ya Mhe. Waziri Prof. Makame Mbarawa na Katibu Mkuu wetu, Balozi Dkt. Aisha Amour, kwa kweli ni timu ya ushindi, ni timu ambayo inatusaidia inatuwezesha kufanya haya mambo na kwa ujumla inatuwezesha kuwahudumia Watanzania kwa ubora na ufanisi zaidi.” Amemaliza Kilahala.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Songoro, Major Songoro ametoa shukrani kwa TEMESA na Serikali kwa ujumla kwa utekelezaji wa miradi hiyo huku wakitoa kipaumbele kwa kampuni za Wazawa kutekeleza miradi hiyo kwani inasaidia kampuni hizo za wazawa kutoa ajira kwa vijana wa Kitanzania. Songoro amesema kwa sasa mafundi wake wanaendelea kufunga mifumo mbalimbali ikiwemo ufungaji wa mifumo ya haidroliki ambayo inatumika kunyanyua na kushusha milango ya kivuko, mifumo ya mabomba, mifumo ya zimamoto pamoja na mifumo ya utoaji maji taka kwenye vivuko.
Aidha, Meneja wa Vivuko Kanda ya Ziwa na Magharibi Mhandisi Vitalis Bilauri amesema wataendelea kumsimamia mkandarasi kwa ukaribu zaidi ili aweze kukamilisha ujenzi wa vivuko hivyo kwa wakati na ndani ya muda uliopangwa.
Ujenzi wa vivuko hivyo vipya na ukarabati wa vivuko pamoja na miundombinu yake ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala cha Mapinduzi ya mwaka 2020/2025.