Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Ujenzi MV Mwanza Wafikia 98%, Yatarajiwa Kuleta Mapinduzi ya Kiuchumi
May 03, 2025
Ujenzi MV Mwanza Wafikia 98%, Yatarajiwa Kuleta Mapinduzi ya Kiuchumi
Muonekano wa meli mpya ya Mv Mwanza inayoendelea kujengwa mkoani Mwanza
Na Jacquiline Mrisho, MAELEZO

Meli mpya ya MV Mwanza inayoendelea kujengwa jijini Mwanza, imetajwa kuleta mapinduzi ya kiuchumi nchini kutokana na fursa mbalimbali zitakazojitokeza kupitia meli hiyo ambayo itaunganisha nchi za jirani za Kenya na Uganda.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa ameyasema hayo jana Mei 02, 2025 jijini Mwanza wakati akizungumza na Waandishi wa Habari wa mkoa wa Mwanza na Shinyanga kwenye ziara iliyolenga kujionea utekelezaji na maendeleo ya miradi mikubwa ya Serikali ikiwemo ujenzi wa meli mpya ya MV Mwanza.

Bw. Msigwa amesema kuwa, ujenzi wa meli hiyo ni uwekezaji uliolenga kuboresha usafiri na usafirishaji wa mizigo katika ziwa Victoria ambapo urahisi wa usafiri katika ziwa hilo utaleta uhakika wa kukua kwa uchumi.

"Meli hii italeta mapinduzi ya uchumi wa Kanda ya Ziwa, hili pia lilikuwa lengo la Serikali kwamba tunajenga meli katika maziwa yetu makubwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa ili kuwa na vyombo vya usafiri wa kwenye maji vinavyoweza kutuunganisha na nchi jirani hali itakayowezesha wananchi kunufaika na fursa za uwepo wa nchi jirani, hivyo kukuza uchumi pamoja na kufungua fursa zingine mbalimbali", amesema Bw. Msigwa.

Kwa upande mwingine, Bw. Msigwa ametoa rai kwa wataalamu wazalendo kujipanga vyema ili kuhakikisha  meli hiyo inadumu muda mrefu kwani itakuwa haina maana kama viongozi wamewezesha maono makubwa kutokea halafu baada ya muda mfupi meli ikaharibika.

Ameeleza kuwa, ni vizuri kila mmoja anayehusika kwenye miradi hiyo mikubwa akaona wajibu wake na  akajipanga kuhakikisha miradi hiyo inakuwa endelevu na kuwanufaisha Watanzania wote.

Akizungumza kuhusu mradi huo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO), Neema Mwale amesema ujenzi wa meli hiyo unagharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100 na itakapokamilika itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo, magari madogo 20 na malori 3.

"Gharama za utekelezaji wa mradi huu hadi kukamilika kwake zitakuwa ni jumla ya shilingi bilioni 139, kwa sasa mradi huu umefikia asilimia 98 ya utekelezaji wake.

Mradi huu unatarajiwa kukamilika kabla au ifikapo tarehe 31 Mei, 2025", amesema Bi. Neema.

Ameeleza kuwa, meli hiyo itakapokamilika inatarajiwa kufanya safari zake kati ya miji ya Mwanza, Musoma, Bukoba kupitia bandari ya Kemondo Bay na nchi jirani za Uganda na Kenya.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi