[caption id="attachment_41448" align="aligncenter" width="750"]
Na. Immaculate Makilika-MAELEZO
Ujenzi wa majengo ya Wizara kwenye Mji wa Serikali uliopo Ihumwa jijini Dodoma umekamilika kwa asilimia 99 ambapo wizara 20 zinatarajia kuhamia ifikapo mwezi Aprili mwaka huu.
Akizungumza leo mara baada ya kufanya ziara katika mji huo, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuwa ujenzi kwenye mji huo umekamilika kwa asilimia 99, aidha amezitaka wizara hizo kukamilisha sehemu ndogo zilizobaki kabla ya mwezi Aprili mwaka huu, ikiwa ni baada ya kupata hati kutoka Wakala wa Ujenzi (TBA).
Waziri Mkuu Majaliwa amesema, “kwa ujumla kazi ni nzuri na imefanywa kwa umakini mkubwa, jukumu lililobaki ni kuhakikisha Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wanaweka umeme wenye nguvu na wakutosha, barabara zote zipitike kwa urahisi, na lazima kuwepo na huduma muhimu ikiwemo kituo cha afya, hoteli, stendi ya daladala na maduka ili watumiaji wa majengo haya waweze kupata huduma hizo”.
[caption id="attachment_41449" align="aligncenter" width="750"]Vile vile ameagiza Makatibu Wakuu wa wizara zote kuhakikisha wanajenga uzio, ikiwa ni sambamba na kuweka mageti yatakayowarahisishia wananchi kufikia ofisi hizo kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali. Huku akiwapongeza TBA, pamoja na wakandarasi mbalimbali walioshiriki katika ujenzi huo.
Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa aliongeza kuwa “watanzania wengi wamenufaika kwa kuwepo kwa miradi hii, kwa vile ujenzi huu na mingine inayoendelea imesaidia kupanua wigo wa fursa kwa Watanzania”.
Naye, Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Wazee na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alisema kuwa huduma mbalimbali zinaendelea kuimarishwa katika mji huo wa Serikali ikiwemo ujenzi wa barabara ambapo Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARULA) na Halmashauri ya Jiji wanaendelea na ujenzi wa kilomita 18 kati ya kilomita 39 zi;izopo ndani ya mji huo wa Serikali.
[caption id="attachment_41450" align="aligncenter" width="750"]Maeneo mengine ni usafiri na mgahawa, ambapo Halmashauri zimeshaanza zoezi la kukamilisha viwango vya nauli kutoka maeneo mbalimbali kuelekea mji wa Serikali.
Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Wazee na Wenye Ulemavu, Mhagama, alisema kuwa “tayari Wizara ya Fedha imeshatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya pamoja na ununuzi wa gari la wagonjwa litakalotoa huduma kituoni hapo”
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani alisema kuwa wizara yake kupitia TANESCO itafunga transfoma yenye ukubwa wa KVA 300 katika mji huo wa Serikali ili kuweza kutoa huduma ya umeme kwa wizara mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kupitisha nyaya za umeme ardhini badala ya nyaya hizo kuonekana juu ya ardhi.
Ujenzi wa Mji wa Serikali ni moja ya agizo la Rais Dkt. John Pombe Magufuli ambapo alizitaka wizara zote kujenga ofisi zake katika mji huo na kuhamia mapema iwezekanavyo ili kuwarahisishia wananchi kupata huduma zote za Serikali katika eneo moja.
[caption id="attachment_41451" align="aligncenter" width="750"]