Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Uhusiano wa Tanzania, China Wakuza Biashara na Uwekezaji Nchini
Jan 06, 2021
Na Msemaji Mkuu

Na Immaculate Makilika- MAELEZO, Chato

Nchi za Tanzania na China zimekuwa na uhusiano wa kiuchumi tangu miaka ya 1970.Katika kipindi cha miaka 40 iliyopita, kufuatia kufungua milango na kufuata sera zauchumi wa soko (Reform and Open Up Policy)  China  imeongeza uzalishaji wa malighafi na bidhaa za viwandani ambazo zimetoa mchango mkubwa katika uchumi wa nchi hiyo sambamba na kupunguza umaskini kwa wananchi wengi.

Hatua hiyo imeiwezesha nchi ya China kuanzisha maeneo mbalimbali ya ushirikiano na Tanzania katika uchumi ambapokwa kipindi cha miaka thelathini (1990-2020), Tanzania imepokea miradi ya uwekezaji kutoka China.

Kwa mujibu wa takwimu za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kwa upande wa Tanzania Bara, jumla ya miradi 940 ya sekta mbalimbali kama vile utalii, kilimo, fedha, ujenzi, viwanda na madini kutoka nchini China yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 7.5 ilisajiliwa katika kituo hicho ambayo imezalisha ajira 117,810. Kwa upande wa Zanzibar, jumla ya miradi nane yenye thamani ya dola za Marekani milioni 142.9 imesajiliwa katika Mamlaka ya Uhamasishaji wa Uwekezeji Zanzibar (ZIPA). Miradi hiyo inahusu uwekezaji katika sekta za viwanda, makazi (real estate), kilimo na uvuvi. 

Aidha, Tanzania ina nafasi kubwa ya kuvutia uwekezaji kutoka China kwa sababu nimiongoni mwa nchi nne za Afrika zilizopewa kipaumbele kunufaika na mpango wa China wa kuhamishia viwanda barani Afrika ujulikanao kama Production Capacity Cooperation Program (PCCP) chini ya Jukwaa laFOCAC na mpango mpya wa One Belt, One Roadambao umelenga kukuza muunganiko wa sera na miundombinu ya kiuchumi na kijamii kati ya China na nchi mbalimbaliulimwenguni.

Halikadhalikatakwimu zinaonesha katika kipindi cha miaka mitano (2014-2018) mauzo ya bidhaa za Tanzania katika soko la China yamefikia wastani wa dola za Marekanimilioni 145 kwa mwaka.  Katika kipindi hicho, Serikali imeweza kufungua fursa mpya za kuuza bidhaa mbalimbali katika soko la China ikiwemo zao la muhogo, mazao ya baharini, mabondo ya samaki, pembe za ng’ombe, mashudu na maharage ya soya.

Katika jitihada za kuimarisha biashara kati ya nchi hizi mbili, Ubalozi wa Tanzania nchini China umeendelea na mkakati wa kutumia vyombo vya habari vya China pamoja na mitandao ya kijamii kutangaza bidhaa za Tanzania katika soko la China.  Vilevile, Ubalozi umeendelea kushiriki katika maonesho mbalimbali ya biashara nchini humo kwa madhumuni ya kutangaza bidhaa za Tanzania.

Kutokana na uhusiano mzuri uliopo baina ya nchi hizi mbili, Tanzania ilipewa fursa ya kuwa miongoni mwa nchi 30 zenye Banda la Taifa (National Pavilion) katika Maonesho ya Pili ya Kimataifa ya Bidhaa za Nje (China International Imports Expo) yaliyofanyika jijini Shanghai Novemba mwaka 2019.  Katika maonesho hayo, banda la Tanzania lilikuwa miongoni mwa mabanda sita yaliyotembelewa na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mheshimiwa XI Jinping, tukio hilo lilioneshwa mubashara katika Vyombo vya Habari vya China na hivyo kufanya bidhaa za Tanzania hususan Tanzanite na Korosho kutangazwa zaidi katika soko la China.

Vilevile, mwezi Juni mwaka 2019, Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi 10 za Afrika zilizopewa Banda la Taifa katika Maonesho ya Kwanza ya Biashara na Uchumi kati ya China na Afrika yaliyofanyika Jijini Changsha katika Jimbo la Hunan.

Ni dhahiri kuwa kutokana na mafanikio ambayo yamekuwa yakipatikana kupitia maonesho hayo, Tanzania inaweza kuongeza ujazo wake wa biashara na China kupitia maonesho ya kimkakati kama vile CAEXPO ambayo hufanyika kila mwaka mwezi Septemba.

Uhusiano mzuri na wa muda mrefu uliopo kati ya China na Tanzania, umesaidia Tanzania kupata fursa ya kushiriki kwa mara ya kwanza kwenye CAEXPO kama mgeni maalum (special partner country) mwezi Septemba 2018. Maonesho mengine ni ya CANTON Fairs ambayo hufanyika mwezi Aprili na Oktoba kila mwaka. Maonesho  ya Biashara na Teknolojia yamekuwa makubwa ambapo mwaka 2018 Chemba ya Biashara ya Wanawake wa Tanzania (TWCC) ilipeleka washiriki 50 kwenye maonesho  hayo kuanzia tarehe 10 hadi 23 Oktoba 2018, vilevile mwaka 2019  TWCC iliandaa ziara ya mafunzo ya wafanyabiashara wanawake 58 kwenye Maonesho ya Canton Fair kuanzia tarehe 8 hadi 18 Aprili, 2019. Aidha, mwaka 2019 Tanzania imeshiriki kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Bustani Beijing (Beijing Horticulture Expo).

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi