Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Uhusiano wa Tanzania-China Ulivyoongeza Idadi ya Wachina Kutalii Nchini
Jan 06, 2021
Na Msemaji Mkuu

Na Immaculate Makilika- MAELEZO, Chato

Idadi ya watalii walioingia nchini imeongezeka kutoka 1,327,143 mwaka 2017 hadi kufikia watalii 1,505,702 mwaka 2018. Ongezeko hilo limechangia kuongezeka kwa mapato yatokanayo na utalii kutoka dola za Marekani bilioni 2.4 mwaka 2018 hadi kufika dola za Marekani bilioni 2.6 mwaka 2019.

Mafanikio hayo yanatokana na jitihada mbalimbali za kutangaza vivutio vya utalii kupitia maonesho ya WTM (Uingereza), ITB (Ujerumani), Conservation and Tourism Fair (Rwanda), Travel Market Top Resa (Ufaransa), Magical Kenya Travel Expo (Kenya), International Tourism Travel Expo (Kanada), China International Expo na Road show (China), Dutch Expo (Uholanzi), Outbond Travel Market - OTM na road show (India), FITUR (Hispania), Holiday Fair (Ubeligiji), na International Mediterranean Tourism Market - IMTM (Israeli) na Falme za Kiarabu

Takwimu za ongezeko hilo zilitolewa na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla, wakati akiwasilisha Bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2020/2021

Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali za kukuza sekta ya utalii nchini ikiwa ni pamoja na kufungua maeneo mapya ya utalii sambamba na kutumia fursa zilizopo mfano uhusiano wa siku nyingi kati ya nchi za Tanzania na china.

Miaka ya hivi karibuni, idadi ya wachina wanaokwenda nchi za nje kutalii imeongezeka kwa kiasi kikubwa kutokana na kukua kwa uchumi wa nchi hiyo na ongezeko la uwezo wa kifedha miongoni mwa wananchi wa China. Mwaka 2016 wachina milioni 120 walisafiri nje ya nchi kutalii sehemu mbalimbali duniani. Inakadiriwa watalii hao walitumia nje ya nchi dola za Marekani bilioni 1.4.

Katika kipindi cha muhula wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Tano, zimefanyika jitihada mbalimbali za kuvutia watalii, Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na wadau wengine katika sekta hiyo wamefanya mikutano ya kutangaza utalii (Tourism Roadshows) katika miji saba ya China ikiwemo Shanghai, Guangzhou, Hong Kong, Beijing, Chengdu, Nanjing na Changsha. 

Mikutano hiyo imewezesha mawakala wa usafiri (Travel Agents) wa China walioshiriki katika mikutano hiyo kupata taarifa za msingi juu ya utalii wa Tanzania na huduma mbalimbali (Tour Packages) zinazotolewa na kampuni za kitalii za hapa nchini. 

Vilevile, Wizara ya Maliasili ana Utalii kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini China, Mhe. Mbelwa Kairuki ilifanya mahojiano na Vyombo vya Habari mbalimbali vya nchini China kuelezea vivutio vya utalii vilivyopo hapa nchini. Halikadhalika Ubalozi uliandaa ziara za waandishi wa habari na mawakala wa safari (Travel Agents) wa China mwezi Oktoba 2018 na mwezi Oktoba 2019. 

Fauka ya hayo, Ubalozi uliweza kuishawishi kampuni ya BAIDU ‘the leading internet search engine in China’ kurusha vipande vya video za kuonesha maeneo mbalimbali ya utalii nchini Tanzania katika mtandao wake.

Jitihada zingine zilizofanyika katika kufungua biashara ya utalii kati ya Tanzania na China ni pamoja na Wizara na Taasisi zinazosimamia utalii  kushiriki kwenye maonesho na makongamano ya kutangaza utalii, kuvutia watu mashuhuri wa China wakiwemo wacheza filamu kutembelea Tanzania na kutumia mitandao kutangaza utalii wa Tanzania ambapo Ubalozi umetengeneza tovuti maalum ya kutangaza utalii kwa lugha ya kichina.

Sambamba na kushawishi Kituo maarufu cha Televisheni cha China (THE TRAVEL CHANNEL) kuja nchini kushiriki maonesho ya utalii ya Swahili International TourismExpo (SITE) yaliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam Oktoba 12 hadi14 , 2018. Maonesho hayo yalihudhuriwa na mawakala wa utalii wapatao 300 kutoka nchi mbalimbali duniani.

Vilevile, baada ya maonesho hayo, kuanzia Oktoba 15 hadi 28, 2018, TTB iliwaandalia waandishi wa habari wa kituo cha hicho kushiriki kwenye ratiba maalum ya kuvitembelea vivutio vya utalii vya hapa nchini na baadaye kuandaa vipindi maalum kuhusu vivutio hivyo kwa ajili ya kuvirusha kwenye televisheni hiyo kwa lengo la kuvitangaza vivutio hivyo katika soko la utalii la China. Waandishi hao walitembelea na kupiga picha katika maeneo ya Dar es salaam, Zanzibar, Dodoma na Kondoa.

Kwa kuzingatia mahitaji ya miundombinu katika mnyororo wa utalii nchini, Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Ubalozi wa Tanzania Beijing kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa utalii imeendelea kuzishawishi kampuni za China kuja kuwekeza kwenye sekta ya utalii ikiwemo ujenzi wa hoteli za kitalii zenye hadhi ya nyota tano. Kampuni zilizoshawishiwa ni pamoja na H&A Group kutoka Jimbo la Hainan, Touchroad International Holding Group kutoka Jiji la Shanghai, na Kampuni ya Tibet Dexin International Financial Leasing Co. Ltd ya China ambayo ina mpango wa kujenga hoteli ya nyota tano yenye vyumba 300 katika eneo la karatu kwa gharama ya dola za Marekani milioni 200.

Mikakati hiyo ya Serikali iliyofanyika kwa kushirikiana na Kampuni ya Touchroad katika kutangaza vivutio vya utalii katika soko jipya la China, mwezi Mei 2019 ilifanikiwa kuratibu mapokezi ya watalii 330 kutoka nchi ya China. Watalii hao 330 walihusisha watu mashuhuri, watumishi wa Serikali, waandishi wa habari, viongozi wa taasisi za utalii na wawekezaji kutoka baadhi ya majimbo tajiri ya China.

Ni dhahiri kuwa kufuatia jitihada hizo, kwa upande wa Tanzania Bara, idadi ya watalii kutoka China imeongezeka kutoka 25,444 kwa mwaka 2015 hadi kufikia 33,541 kwa mwaka 2019.  Kwa upande wa Zanzibar, katika kipindi cha kuanzia 2016 hadi 2020 jumla ya watalii 30,109 walipokelewa kutoka China.

Hata hivyo, kwa kuzingatia ukubwa wa nchi ya China kijiografia na wingi wa idadi ya mawakala wa utalii, Serikali imeendelea kuboresha sekta ya uchukuzi sambamba na kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam kwenda Guangzhu mwanzoni mwa mwaka huu, kwa lengo la kuongeza idadi ya watalii kutoka China.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi