Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Uhuru, Usalama wa Nchi Waimarisha Uchumi
Apr 03, 2024
Uhuru, Usalama wa Nchi Waimarisha Uchumi
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Lawrence Tax akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio ya Wizara hiyo katika kipindi cha miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo Aprili 3, 2024 jijini Dodoma.
Na Lilian Lundo, Maelezo

Wizara ya Ulinzi na Jeshi  la Kujenga Taifa, limechangia kujenga uchumi imara kwa kulinda mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo wananchi kuwa na uhuru wa kufanya shughuli za uzalishaji mali bila hofu.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Stergomena Tax, amesema hayo leo Aprili 3, 2024 jijini Dodoma, wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Katika kulinda mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uhuru na usalama wa nchi, wizara kupitia JWTZ imechangia katika kujenga uchumi imara ambapo wananchi hujishughulisha na shughuli za uzalishaji mali bila hofu,” amesema Mhe. Stergomena.

Ameendelea kusema kuwa, hayo yote yamewezekana kutokana na kuwepo kwa sera, sheria, kanuni na mipango madhubuti katika ulinzi wa nchi, vinavyotoa fursa kwa wananchi kujikita katika ujenzi wa taifa lao. 

Aidha, serikali kupitia wizara hiyo imeendelea kutekeleza, na kuliimarisha jeshi kwa kulipatia zana na vifaa bora na vya kisasa, rasilimali watu, na nyenzo za kufanyia mazoezi ili kuwa imara wakati wote. 

“Mafanikio mengine ni ushiriki wa wizara kupitia taasisi zake, hususan JWTZ katika kukabiliana na majanga au maafa mbalimbali pale yanapotokea. Katika kutekeleza jukumu hilo, JWTZ imeendelea kushiriki kikamilifu katika kutoa misaada ya uokoaji na ile ya kibinadamu kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa,” amesema Mhe. Stergomena

Aidha, wizara kupitia JWTZ imeendelea kushirikiana na mamlaka za kiraia katika miradi ya kimkakati. Baadhi ya maeneo ambayo JWTZ imeshirikiana na mamlaka za kiraia ni pamoja na kushiriki katika kuboresha huduma katika taasisi za Serikali; kushiriki katika ulinzi wa miradi na maeneo ya kimkakati kwa nchi ikiwemo katika migodi mbalimbali, ulinzi wa miundombinu kama Reli, ikiwa ni pamoja na reli ya Kisasa Standard Gauge Railway (SGR).

Miradi mingine ni Bwawa la kufua Umeme wa Maji la Julius Nyerere (Julius Nyerere Hydro Power Project - JNHPP); ulinzi katika Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Kampuni ya Simu (TTCL), na maeneo ya viwanja vya ndege. 

Eneo lingine ni utoaji wa huduma za afya na tiba kupitia hospitali za jeshi za kanda ambazo ni Lugalo, Dar es Salaam; MH, Mwanza; Bububu, Zanzibar; Mirambo, Tabora; MH, Arusha; MH Mbeya ambazo hutoa huduma kwa wanajeshi, na pia kwa wananchi waishio maeneo yaliyo jirani na kambi za jeshi, na katika hospitali nyingine, ambapo takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya wanaopata huduma katika hospitali za Jeshi ni raia.


 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi