Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Udugu wa Damu Kati ya Wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar, Sababu Moja Wapo ya Muungano - Waziri Jafo
Apr 14, 2024
Udugu wa Damu Kati ya Wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar, Sababu Moja Wapo ya Muungano - Waziri Jafo
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo akizungumza wakati wa uzinduzi wa Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar katika viwanja vya Maonesho ya Biashara Nyamanzi Wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa Mjini Magharibi leo Aprili 14, 2024 ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Na Mwandishi Wetu

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema miongoni mwa sababu za Muungano wa Tanzania ni udugu wa damu kati ya wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar.

Amesema wananchi wa pande mbili za muungano wameunganishwa na lugha adhimu ya Kiswahili ambayo imejenga urafiki kati yao chini ya waasisi Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Amani Karume.

Dkt. Jafo amesema hayo wakati wa uzinduzi wa Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar katika viwanja vya Maonesho ya Biashara Nyamanzi Wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa Mjini Magharibi leo Aprili 14, 2024 ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Akizungumzia historia fupi ya Muungano, Dkt. Jafo amesema kuwa hadi kufikia kusaini Hati ya Muungano, viongozi hao wawili waliunganishwa na vyama vya TANU kwa upande wa Tanzania Bara na ASP kwa upande wa Zanzibar ambavyo vilitoa mchango mkubwa katika muungano.

Hivyo, amesema kuwa katika kilele cha miaka 60 ya muungano, kitabu cha Historia ya Muungano kitazinduliwa ili kuijengea jamii uelewa zaidi kuhusu wapi tulipotoka na wapi tunaelekea huku tukidumisha muungano huu adhimu.

Ametoa pongezi kwa viongozi wakuu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuendelea kusimamia utatuzi wa hoja za muungano katika kipindi kifupi cha uongozi wao.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla na viongozi kutoka ofisi ya Makamu wa Rais.

 

Maadhimisho ya miaka 60 ya muungano yamechagizwa na kaulimbiu, “Tumeshikamana na Tumeimarika kwa Maendeleo ya Taifa Letu”, ambapo kilele kitakuwa Aprili 26, 2024 kwenye uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. 

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi