Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

UCSAF Yatoa Ruzuku ya Tsh. Bilioni 93.3 Kwa Makampuni ya Simu.
Sep 27, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na: Mwandishi Wetu

SERIKALI kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote imetoa ruzuku ya Tsh Bilioni 93.3 kwa makampuni ya simu za mkononi kwa ajili ya kujenga minara ya mawasiliano ili kufikisha huduma za mawasiliano katika kata 518 nchini hatua inayolenga kuchochea ukuaji wa uchumi na utoaji wa huduma za kijamii kwa wananchi.

Hayo yameelezwa hivi karibuni na Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Mhandisi Peter Ulanga wakati wa ziara iliyoandaliwa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia UCSAF ya kuwapeleka wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu kukagua maendeleo ya ujenzi wa minara ya simu za mkononi, hali ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi pamoja na changamoto zilizopo.

Mhandisi Ulanga aliongeza kuwa Serikali kupitia UCSAF inaendelea kutoa ruzuku kwa kampuni za simu za mkononi  ili ziweze kufikisha mawasiliano kwenye vijiji vyote nchini, ambapo hadi sasa jumla ya kata 391 kati ya kata 518 zimefikishiwa huduma ya mawasiliano katika kipindi cha miaka minne kuanzia mwezi Machi 2013 mpaka mwezi Agosti 2017 mwaka huu.

Wakiwa katika kata ya Jipe Wilaya ya Mwanga mkoa wa Kilimanjaro Mhandisi Ulanga alisema kuwa mnara wa Vodacom uliojengwa kwenye eneo hilo unahudumia zaidi ya wananchi 1,200 kwenye vijiji zaidi ya nane, ambapo hata hivyo hadi sasa UCSAF imejenga minara ya simu za mkononi katika maeneo saba yaliyopo Wilaya ya Mwanga na Same mkoani Kilimanjaro kwa kushirikiana na kampuni za simu za mkononi.

Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa aliyefanya ziara katika Wilaya za Bahi na Chamwino mkoani Dodoma pamoja na Gairo Mkoani Morogoro, ameziagiza kampuni za simu kuhakikisha kuwa huduma za mawasiliano vijijini zinapatikana masaa 24, katika siku saba za wiki na katika kipindi cha mwaka mzima

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Prof. Norman Sigalla alisema kamati yake itaendelea kuhakikisha kuwa Serikali inafikisha huduma za mawasiiano vijijini kwa wananchi wote mikoa mbali mbali nchini.

Prof. King aliongeza kuwa wananchi wa vijiji mbalimbali washirikiane na kampuni za simu kulinda miundombinu ya mawasiliano ili waendelee kunufaika na uwepo wa minara hiyo kwenye makazi yao.

Aidha, ujenzi, usimikaji wa minara na ufikishaji wa huduma za mawasiliano vijijini zimekuwa zikifanywa kwa pamoja kati ya Serikali na kampuni za simu za mkononi ikiwemo Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Airtel, MIC TIGO, Vodacom, Zantel na Halotel.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi