Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania hususan wakazi wa Wilaya ya Mkalama mkoani Singida Kutunza Amani na Utulivu uliopo nchini hasa katika kipindi hiki ambapo nchi inajiandaa kuingia kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa ifikapo 2024.
Rais Samia alisema hayo leo Oktoba 16, 2023 ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake mkoani Singida, ambapo pamoja na mambo mengine alifungua daraja na msingi na kuzungumza na wakazi wa eneo hilo ambapo aliwasihi kujitahidi kuepusha makundi pamoja na kuchagua watu ambao watawatumika badala ya kuwagawanya.
“Tunapoelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwakani, nawaomba mchague viongozi watakaowatumikia, tujitahidi kujiepusha na makundi, uchaguzi pia una mkono wa Mungu, unaweza ukaitaka nafasi ya uongozi lakini Mungu hakukupangia, hivyo unapokosa usianze kutengeneza makundi tukaanza kubomoa chama chetu, kuweka chuki na kufanya maendeleo yasipatikane, nawaomba dumisheni, upendo, umoja na mshikamano tufanye chaguzi zetu vizuri,” alisema Rais Samia.
Akiongelea suala la daraja alilolizindua Rais Samia alisema Daraja la Msingi lina umuhimu mkubwa kwa shughuli za usafiri na usafirishaji kati ya Mkoa wa Singida na mikoa jirani ya Simiyu, Mwanza, Mara, Manyara, Arusha pamoja na maeneo mengine, alisema daraja hilo ni kiungo muhimu kati ya ukanda wa kati na nchi za Afrika Mashariki hususan kwenye mpaka wa Sirari.
“Ni matumaini yangu kuwa uwepo wa daraja hili na madaraja yote yaliyojengwa yatachochea zaidi biashara ya mazao ya kilimo, ufugaji pamoja na bidhaa kutoka kwenye viwanda vidogo vidogo, natoa wito kwenu kufanya kazi kwa bidii ili muweze kuona manufaa ya daraja hili, nasisitiza kutunza miundombinu yote iliyojengwa ili iweze kutufaa leo na huko tunakoenda,” alisema Rais Samia.