Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tunaweka Mikakati Kulinda Bunifu za Vijana Katika TEHAMA - Wizara
Oct 17, 2023
Tunaweka Mikakati Kulinda Bunifu za Vijana Katika TEHAMA - Wizara
Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Mifumo na Huduma za TEHAMA, Bw. Mohamed Mashaka akizungumza katika mkutano wa vijana wanaojihusisha na mifumo ya teknolojia ya habari na mawasiliano, ambao ni sehemu ya Kongamano la saba la TEHAMA 2023, litakalofanyika Oktoba 18-20 Jijini Dar es Salaam.
Na Grace Semfuko, MAELEZO

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imesema inaweka mikakati ya kulinda bunifu za kiteknolojia za mawasiliano zinazotengenezwa na vijana nchini ili kuwawezesha kuwa na ubunifu zaidi, na kujikwamua kiuchumi kupitia kazi zao.

Hayo yamebainishwa leo Oktoba 17, 2023 na Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Mifumo na Huduma za TEHAMA, Bw. Mohamed Mashaka, katika mkutano wa vijana wanaojihusisha na mifumo ya teknolojia ya habari na mawasiliano, ambao ni sehemu ya Kongamano la saba la TEHAMA 2023, litakalofanyika Oktoba 18-20 Jijini Dar es Salaam.

“Kama Wizara tuna jitihada mbalimbali tunazifanya kuhakikisha tunalinda bunifu za vijana, kwanza tunatengeneza sera ambayo itatoa mwongozo jinsi gani hizi bunifu zitakuwa zinalindwa, hapa tuna mambo manne, ambayo ni kuzitambua zile teknolojia za ubunifu, kulinda zile bunifu kwa sababu leo hii mtu anaweza kutengeneza teknolojia nzuri lakini watu wenye hela wanakuja kuzichukua” amesema Bw. Mashaka

Amesema pia mkakati huo utasaidia kuzitangaza bunifu hizo za vijana ili zisipotee na pia kuziendeleza.

“Jambo lingine ambalo ni muhimu sana ni namna ya kuziendeleza hizo bunifu, mara nyingi mtu anakuja na ubunifu mzuri sana, lakini baada ya muda mfupi unakufa, sasa lazima tuziwekee uendelevu, yaani teknolojia hiyo iendelee kuishi, hayo ndiyo maeneo manne makubwa ambayo sisi wizara tumeona tukiyaendeleza vizuri tutaleta maendeleo makubwa ya kidigitali Tanzania,” amesema Bw. Mashaka.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi