Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tunaishukuru Serikali ya Cuba Kwa Kutambua Mashujaa wa Afrika - Majaliwa
Aug 26, 2017
Na Msemaji Mkuu

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameishukuru Serikali ya Cuba kwa kutambua na kuthamini mchango mkubwa uliotolewa na mashujaa wa ukombozi wa Bara la Afrika, akiwemo Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere kwa kuwajengea mnara wa kumbukumbu.

Mnara huo umejengwa katika Manispaa ya Playa jijini Havana kwenye eneo maalumu la makumbusho ya mashujaa hao walioshiriki katika ukombozi wa Afrika, ambapo  zimewekwa sanamu zao pamoja na maelezo mafupi ya historia zao na nchi wanazotoka.

Waziri Mkuu alifanya ziara katika eneo hilo jana (Ijumaa, Agosti 25, 2017) na kuweka shada la maua katika mnara huo uliozungukwa na sanamu za mashajuaa wa Bara la Afrika na kuoneshwa sehemu itakayowekwa sanamu ya Mwl. Nyerere.

Akiwa katika eneo hilo, Waziri Mkuu aliishukuru Serikali ya Cuba kwa kujenga makumbusho ya mashujaa hao na kwamba Serikali ya Tanzania itashirikiana na Cuba kuhakikisha kuwa sanamu ya Mwl. Nyerere inawekwa katika sehemu iliyotengwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Instuto Cubano De Amistad Con El Pueblo (Taasisi ya Ushirikiano wa Cuba na Nchi Marafiki), Bw. Jose’ Prieto Cintado alisema mnara huo umejengwa kwa lengo la kutambua thamani na umuhimu wa viongozi hao.

Mkurugenzi huyo alisema Serikali ya Cuba inathamini mchango mkubwa uliotolewa na mashujaa hao katika vita ya ukombozi wa Bara la Afrika, ambapo iliamua kujenga mnara wa kumbukumbu katika nchi yao.

 Alisema wananchi wa Cuba pamoja na watu kutoka mataifa mbalimbali ndani na nje ya Bara la Afrika wanakwenda katika eneo hilo la makumbusho na kujifunza historia za viongozi hao. Pia eneo hilo linatumiwa na watafiti wa masuala ya kihistoria.

Mashujaa ambao tayari sanamu zao zimekwishawekwa kwenye eneo la kuzunguka mnara huo ni pamoja na Jomo Kenyatta (Rais wa kwanza wa Kenya), Modibo Keita (Rais wa Mali), Amilcar Cabral (Rais wa kwanza wa Guinea Bissau).

Wengine ni  Dkt. Kwame Nkrumah (Rais wa kwanza Ghana), Oliver Thambo (Kiongozi Mwandamizi wa Chama cha Ukombozi cha ANC cha Afrika Kusini), Eduardo Chivambo Mondlane (Kiongozi wa ukombozi nchini Msumbuji).

Wengine ni Samora Moises Machel (Rais wa kwanza wa Msumbuji), Sekou Toure (Rais wa kwanza wa Senegal), Seretse Khama (Rais wa kwanza wa Botswana), Alhaji Aboubakar Tafawa Balewa na Obafemi Jeremiah Awolowo (Mawaziri Wakuu wa zamani wa Nigeria) na Chifu Jeremia Azikiwe (Rais wa zamani wa Nigeria)  .

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

JUMAMOSI, AGOSTI 26, 2017.

 

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi