Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tumieni Fursa za Utafiti wa Madini na Mafunzo Kupitia AMGC- Prof. Mdoe
Sep 13, 2017
Na Msemaji Mkuu

Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe akiongea wakati wa Mkutano wa 37 wa mwaka wa Kituo cha Madini Afrika uliofanyika leo Kunduchi jijini Dar es Salaam.

Jonas Kamaleki- MAELEZO

Watanzania wametakiwa kutumia fursa zinazopatikana katika kituo cha Afrika cha Sayansi ya Jiolojia na Madini (AMGC) ikiwemo kutumia maabara za kisasa za uchunguzi wa madini.

Rai hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Prof. James Mdoe wakati wa kikao cha Makatibu Wakuu, Makamishina wa Madini wa nchi wanachama wa kituo hicho.

“Wanafunzi wa vyuo vikuu wameanza kutumia kituo hiki katika masomo yao kitu ambacho ni faida ya uwepo wa kituo hiki muhimu barani Afrika hapa nchini,”alisema Profesa Mdoe.

Baadhi ya wawakilishi wa Bodi ya Kituo cha Afrika cha Sayansi ya Jiolojia na Madini (AMGC). Kutoka kulia ni Mwenyekiti wa UNECA, Dkt. Koja Busia, Mwenyekiti wa Bodi, Masresha Gebreselassie, Mwenyekiti wa AUC, Frank Mugyenyi na Mkurugenzi Mkuu wa AMGC, Ibrahim Shaddad.

Prof. Mdoe amezitaja kazi za kituo hicho kuwa ni kufanya utafiti na kuongeza thamani ya madini, kutoa mafunzo na ushauri wa masuala ya madini na kuhifadhi na kusambaza taarifa za madini zinazohusu nchi wanachama na kuweka kanzidata ya madini.

Licha ya mafanikio yaliyopatikana ndani ya miaka arobaini tangu uanzishwaji wa AMGC, zipo changamoto ambazo zinakikabili kituo hicho kama Prof. Mdoe alivyoainisha kuwa ni pamoja na kutolipa michango ya uanachama kwa wakati jambo ambalo linazorotesha utendaji wa kazi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa AMGC, Bw. Ibrahim Shaddad amezitaka nchi za kiafrika ambazo hazijajiunga, kujiunga ili kupata manufaa ambayo yanapatikana kwenye kituo hicho.

Aidha, Shaddad amesema Kituo kimeanza kutafuta namna ya kujiendesha ili kuepukana na kutegemea michango ya wanachama ambayo haikidhi haja na matakwa ya AMGC.

Mshauri Mwelekezi wa AMGC, Timo Gawronski akitoa maelezo kwa washiriki wa kikao wakiwa  katika maabara ya uchunguzi wa asili  ya madini husika.

Amewahamisisha nchi wanachama kutumia maabara za kisasa zilizopo kituoni hapo na huduma nyingine kama vile mafunzo na ushauri ili kupata manufaa yatokanayo na kituo hicho.

Kituo hiki ambacho ni cha kipekee barani Afrika kwenye utafiti na uchunguzi wa Madini mwaka huu kinatimiza miaka 40 tangu kuanzishwa kwake. Kwa sasa kina jumla ya nchi wanachama nane zikiwemo, Angola, Kenya, Burundi, Uganda, Sudan, Ethiopia, Msumbiji na wenyeji Tanzania.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi