Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tume ya TEHAMA Kuendelea Kukuza Shughuli za TEHAMA
Aug 27, 2023
Tume ya TEHAMA Kuendelea Kukuza Shughuli za TEHAMA
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga akizungumza Agosti 25, 2023 katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO uliopo jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa Tume hiyo na mwelekeo wake kwa Mwaka wa Fedha 2023/24.
Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO

Vipaumbele mbalimbali vilivyowekwa na Tume ya TEHAMA katika mwaka wa fedha 2023/24, vinatarajiwa kuendelea kukuza shughuli za TEHAMA na uchumi wa kidijitali nchini ikiwa ni utekelezaji wa moja ya  jukumu la Tume hiyo ya kuifanya Tanzania kushindana kidunia katika utekelezaji shughuli za TEHAMA.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga amesema hayo Agosti 25, 2023 katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO uliopo jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa Tume hiyo na mwelekeo wake kwa Mwaka wa Fedha 2023/24.

Dkt. Mwasaga amesema kuwa, TEHAMA imesaidia masuala mbalimbali hapa nchini na hivyo kufanikiwa kwa kiwango kikubwa katika TEHAMA kwani kampuni mbalimbali zimetengeneza mitaji mikubwa na zinafanya kazi nchi nyingi duniani.

"Vipaumbele vya Tume hii ni kuendelea na ukamilishwaji wa vituo vya ubunifu TEHAMA katika Kanda 5 pamoja na kuanzisha kituo kimoja Zanzibar, kuanzisha kituo cha kutengeneza na kuboresha vifaa vya TEHAMA, kuratibu na kuandaa matukio ya kuvutia uwekezaji na kutangaza masoko ya bidhaa za TEHAMA ndani na nje ya nchi, kuwezesha uanzishaji wa vituo vya majaribio vya ubunifu TEHAMA katika Wilaya 10 pamoja na kuanzisha Kituo cha “Resilience Academy” hapa nchini", amesema Dkt. Mwasaga.

Ameongeza kuwa, Tume itafanya tafiti za maendeleo ya TEHAMA nchini na kufanya tathmini ya kitaifa ya hatua za utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya TEHAMA, itafanya tafiti za maendeleo ya TEHAMA kwa kila wilaya itashirikiana na washirika wa maendeleo na kampuni za kimataifa katika kuendeleza bunifu za TEHAMA ikiwemo kuwezesha utengenezaji wa bidhaa za TEHAMA hapa nchini pamoja na kujenga kituo cha Akili Bandia “Artificial Intelligence” kwa ajili ya kuendeleza wataalam wa TEHAMA.

Vilevile, Tume itawezesha mafunzo maalum ya wataalam wa TEHAMA 500, kukuza soko la bidhaa na huduma za kampuni ndogondogo, kuratibu na kutengeneza mfumo wa usimamizi wa utekelezaji wa Sera ya TEHAMA na kufanya tafiti za kuweza kufanya maboresho ya sera kulingana na mabadiliko ya teknolojia, kujenga “metaverse studio” kwa ajili ya kutengeneza maudhui ya metaverse na pia kuboresha maudhui ya mitandao.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi