Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TRA Yawahimiza Wafanyabiashara, Wamiliki wa Majengo Kulipa Kodi kwa Wakati
Mar 13, 2019
Na Msemaji Mkuu

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewahimiza wafanyabiashara na wamiliki wa majengo kote nchini kulipa kodi kwa wakati hususani Kodi ya Mapato awamu ya kwanza, Kodi ya Majengo na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambapo huu ndio muda muafaka wa kulipa kodi hizo.

Akizungumza na walipakodi katika Ofisi za TRA Vingunguti jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi, Richard Kayombo amesema kodi ya ongezeko la thamani inatakiwa kulipwa ifikapo Machi 20 mwaka huu, kodi ya mapato inatakiwa kulipwa kabla ya tarehe 30 Machi, 2019 wakati mwisho wa kulipa kodi ya majengo ni mwezi Juni, 2019.

“Ninachukua fursa hii kuwahimiza wafanyabiashara na wamiliki wa majengo mliopo hapa na wale watakaosikia taarifa hii kwenye vyombo mbalimbali vya habari kuwahi kulipa kodi hizi kwa wakati ili kuepuka usumbufu na hatimaye kujikuta mnatozwa faini na riba," alisema Kayombo.

Amesema kuwa, viwango vya kodi ya majengo ni shilingi 10,000 kwa nyumba za kawaida, shilingi 50,000 kwa kila sakafu ya ghorofa na shilingi 20,000 kwa nyumba za ghorafa zilizoko vijijini.

"Tunaona serikali imepunguza kiwango cha kodi ya majengo, hivyo hakuna sababu ya watu kuchelewesha na kusubiri dakika za mwisho, tulifanye suala la ulipaji kodi kuwa utamaduni wetu kwa lengo la kuleta maendeleo ya nchi yetu,” alisisitiza Kayombo.

Wakati huo huo, Mkurugenzi Kayombo amewatahadharisha walipakodi kuhusu uwepo wa watu wanaotumia jina la mamlaka hiyo kufanya utapeli kwa kujitambulisha kuwa ni maofisa wa TRA wakidai kwenda kukagua ulipaji wao wa kodi.

“TRA ina utaratibu wake wa kuwasiliana na wafanyabiashara na kuwajulisha siku rasmi ambazo maofisa wetu watakwenda kufanya ukaguzi na unafanyika kwa uwazi bila vitisho na si kwa taratibu nyinginezo,”alisema Kayombo

Ameongeza kuwa, "kama  mtu atapigiwa simu au kama una mtu una wasiwasi nae tafadhali toa taarifa kwa ofisi zetu zilizopo karibu nawe au toa taarifa Kituo cha Huduma kwa Wateja  namba 0800 780 078 au 0800 750 075 kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa moja usiku na utupe namba ya mhusika ili tuweze kufuatilia.

“Pia kuna namba ya Whatsapp ambayo unaweza kutoa taarifa au kuuliza chochote kupitia namba 0744 233 333 ambayo ni maalum kwa ajili ya kutatua changamoto za wananchi na kuwawezesha kulipa kodi kwa wakati,” alisema Kayombo.

Richard Kayombo amesema kuwa, tangu mwezi Desemba mwaka jana, TRA imekuwa ikipata malalamiko kutoka kwa watu tofauti tofauti ambao wamekuwa wakitapeliwa fedha na maofisa feki wanaodai kufanya kazi Mamlaka ya Mapato Tanzania.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi