Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TRA Yaja na Mikakati Mipya Ya Ukusanyaji Kodi
Apr 25, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na Husna Saidi na Nuru Juma- MAELEZO

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya Trilioni 10.87 mpaka kufikia Machi mwaka huu kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hayo yamesemwa na Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo Charles Edward Kichere wakati wa  mahojiano na mtangazaji wa TBC1 Rashid Salum katika kipindi cha Tunatekeleza kinachorushwa  kila siku za Jumatatu saa moja kamili jioni na Alhamisi saa tatu na nusu usiku.

Kichere alisema, mwaka huu wa fedha 2016/2017 TRA inatakiwa kukusanya Trilioni 15.105 na hadi kufikia Machi mwaka huu TRA  imefanikiwa kukusanya Shilingi Trilioni 10.87.

Aliendelea kwa kusema kuwa mpaka kufikia Juni mwaka huu TRA  itahakikisha inatimiza lengo la kukusanya Shilingi Trilioni 15.105 ili kusaidia  Serikali kuleta maendeleo kwa wananchi wake.

Alisema kuwa TRA ina waajiriwa wapya ambao wamepewa mafuzo ya miezi sita katika  chuo cha kodi juu ya mifumo mbalimbali ya ukusanyaji kodi ambao waliajiriwa moja kwa moja na mamlaka hiyo  kwaajili ya kutekeleza majukumu ya ukusanyaji kodi ndani ya nchi.

“Tunatumia mfumo wa Tehama kukusanya kodi na mifumo mingine mbalimbasli  kama  vile Tigo Pesa , Airtel Money na MPesa ili kurahisishia watu kulipa kodi wakiwa nyumbani na kuepuka usumbufu,” alisema Kichere.

Kichere aliongeza kuwa kwa mwaka huu wa fedha mapato yameongezeka mpaka kufikia asilimia 9.9 hadi 10 licha ya kuwa kuna baadhi ya maeneo hawakuweza kukusanya.

Aidha Kichere alisema Mamlaka kwa sasa imejipanga kuwa na mahusiano mazuri na wafanyabiashara ili kuhakikisha wafanyabiashara wanalipa kodi stahiki na kwa mujibu wa sheria bila kutumia nguvu au uonevu wowote.

Hata hivyo mamlaka hiyo imekuwa ikitoa  elimu kwa walipa kodi kwa kupitia vyombo mbalimbali vya habari, kutoa semina kwa watumishi wa umma , kuandaa makongamano ambayo yanatoa elimu, kupitia mitandao ya kijamii na ziara mbalimbali ambazo wamekuwa wakizifanya ili kuhakikisha wafanyabiashara wanapata elimu pamoja na kujua wajibu wao katika kulipa kodi ili kuleat maendeleo nchini.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi