Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TRA: Wananchi Lipeni Kodi ya Majengo, Viwango Vimepunguzwa
Nov 13, 2019
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_48823" align="aligncenter" width="750"] Afisa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Morogoro, Bw. Morgan Njama (kulia) akimuelimisha Mlipakodi wa Kata ya Mlimba mkoani Morogoro wakati wa Wiki ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi mkoani hapo.[/caption]

Na Veronica Kazimoto -Kilombero

Wito umetolewa kwa wananchi kulipa kodi ya majengo kwa kuwa viwango vilivyopangwa katika kodi hiyo ni rafiki na vinalipika kwa urahisi ukilinganisha na hapo awali.

Wito huo umetolewa na Afisa Kodi Mkuu, Julius Mjenga kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakati wa Kampeni ya Usajili, Huduma na Elimu kwa Mlipakodi katika Kata ya Mlimba Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro.

[caption id="attachment_48824" align="aligncenter" width="750"] Afisa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Lameck Ndinda (kushoto) akiwaelimisha Vijana wa Bodaboda wa kata ya Mlimba mkoani Morogoro kuhusu umuhimu wa kuhamisha kadi za vyombo vya moto wakati wa Wiki ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi mkoani hapo.[/caption] [caption id="attachment_48825" align="aligncenter" width="750"] Mfanyabiashara wa kata ya Mlimba mkoani Morogoro, Bibi Justina Rugwana akitoa hoja wakati wa Kampeni ya Huduma, Elimu na Usajili kwa Mlipakodi mkoani hapo.[/caption]

Mjenga amesema kuwa, sasa hivi viwango vya kulipia kodi ya majengo ni shilingi 10,000 kwa nyumba za kawaida, shilingi 50,000 kwa kila sakafu ya ghorofa katika Majiji, Miji na Manispaa na shilingi 20,000 kwa ghorofa zima katika Halmashauri za Wilaya.

“Sasa hivi viwango vimepunguzwa wale wenye nyumba za kawaida wanalipia shilingi 10,000 tu na wale wenye nyumba za ghorofa zilizopo kwenye manispaa, miji na majiji wanalipia shilingi 50,000 kwa kila sakafu wakati wale wenye nyumba za ghorofa zilizopo halmashauri ya wilaya wanalipia shilingi 20,000 kwa ghorofa zima,” alisema Mjenga.

Mjenga amefafanua kuwa katika majiji, manispaa na halmashauri za miji, iwapo kuna nyumba zaidi ya moja kwenye kiwanja kimoja, kila nyumba itatozwa shilingi 10,000 wakati katika halmashauri za wilaya, endapo kiwanja kimoja kina nyumba zaidi ya moja, nyumba yenye thamani ya juu ndio itakayohesabika na kutozwa shilingi 10,000.

[caption id="attachment_48826" align="aligncenter" width="750"] Afisa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Lameck Ndinda (kushoto) akichukua taarifa zilizopo kwenye Cheti cha Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) kwa ajili ya kujiridhisha kama ni ya biashara wakati wa Wiki ya Usajili, Huduma na Elimu kwa Mlipakodi mkoani Morogoro.[/caption]

Aidha, majengo yasiyotozwa kodi ya majengo ni pamoja na nyumba zilizoezekwa kwa nyasi na makuti, nyumba zilizojengwa kwa udongo (nyumba za tope) na majengo ya ibada kama vile misikiti na makanisa.

Julius Mjenga amewataja wazee wenye miaka 60 na kuendelea kuwa wamesamehewa kulipa kodi ya majengo kwa nyumba moja ambayo wanaishi na si vinginevyo na wazee hao wanapaswa kufika Ofisi za TRA kuomba kusamehewa kodi hiyo.

Mamlaka ya Mapato Tanzania inaendelea na kampeni ya usajili, huduma na elimu kwa mlipakodi katika Mikoa ya Morogoro na Pwani na itamalizika tarehe 17 Novemba, 2019.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi