Adeladius Makwega, WHUSM–Dodoma.
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wakishirikiana na Taasisi ya Sekta Binafsi za Tanzania (TPSF) wamekutana kujadili adhima na umuhimu wa kuanzisha baraza la ujuzi la sekta binafsi nchini.
Majadiliano haya yamefanyika Agosti 4, 2021 katika kikao baina ya watendaji wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na TPSF Mtumba Mji wa Kiserikali Jijini Dodoma..
Akizungumzia suala hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sanaa wa Wizara hiyo, Mfaume Said amesema kuwa kuanzishwa kwa baraza hilo itakuwa nafasi ya wadau kujadili na kuwasilisha changamoto zao zilizopo katika sekta ya ubunifu na wataweza kuisadia zaidi Serikali kutokana na yale yanayobainika.
“Pia tutapata uwezo wa kuwa na takwimu sahihi juu ya sekta bunifu hapa nchini na tutaweza kupata soko la kazi za sanaa iwe filamu, muziki, uchongaji, uchoraji, usukaji, ubunifu wa michoro na kazi zingine.” alisema Kaimu Mkurugenzi huyo.
“Hii ni fursa kubwa kwetu na kwa taifa letu kwani tunajiandaa tuwe na makubaliano ya pamoja ya namna tutakavyoifanya kazi hii kwa manufaa ya kila idara iwe ya michezo, utamaduni au Sanaa”,alisisitiza Kaimu Mkurugenzi huyo.
Akizungumza kuhusu majadiliano hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Francis Nanai alisema kuwa hili ni jambo jema kwa kuwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ni mdau namba moja lazima mafanikio haya yatafanikiwa kwa kiwango cha juu .
“Sisi kama TPSF tumepokea fedha kutoka UNESCO kupitia mradi wa BEAR (III) kwa nia moja ya kuhakikisha baraza la ujuzi la sekta bunifu linaazishwa. ndiyo maana tumepiga hodi wizara yetu kuelimishana juu ya faida yake kwa wizara pamoja na wadau wenu.” Alisema Francis Nanai.