Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tiketi Mtandao Kuanza Aprili 2022
Dec 21, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Na Salum Pazzy - LATRA

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara amesema mfumo wa Tiketi Mtandao, utaanza kutumika rasmi Aprili, mwakani.

Amesema hatua hiyo inatokana na kupatiwa ufumbuzi kwa changamoto mbalimbali zilizolalamikiwa na wadau wa sekta hiyo.

Waitara alibainisha hayo jijini Dar es Salaam leo Disemba 20, 2021 katika kikao maalumu cha kupokea taarifa ya kamati ndogo iliyoundwa Julai, mwaka huu, kubainisha changamoto za mfumo wa Tiketi Mtandao na kupendekeza jinsi ya kuzitatua.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, yapo mambo wamekubaliana na wadau ili kuanza kwa mfumo huo na mengine yatahitaji mabadiliko ya sheria na kanuni.

“Tutakaa Wizara, Wamiliki wa Mabasi (TABOA), Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) na Wizara ya Fedha na Mipango na tutayachakata maoni hayo yaliyopendekezwa ili yarekebishwe na tutayafanyia kazi, marekebisho mengine yatahitaji kwenda bungeni,” alisema.

Waitara aliweka bayana kwamba Serikali itaweka mfumo rafiki utakaosaidia kuleta uhusiano mzuri baina ya wamiliki wa mabasi na LATRA ambapo zikitokea changamoto za kiutendaji wazitatue kupitia mfumo bora zaidi.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mkurugenzi wa Huduma za Uchukuzi wa Wizara hiyo, Mhandisi Aron Kisaka, alisema kamati hiyo ilikuwa na wajumbe 11 na wamezifanyia kazi changamoto 17.

“Julai, mwaka huu, Katibu Mkuu wa Uchukuzi aliunda kamati ndogo ya kuainisha changamoto  zinazowapata  wamiliki wa mabasi katika matumizi ya Tiketi Mtandao na  baadaye kutoa ushauri wa namna ya kuzitatua.”

“Kupitia kamati yetu tulibaini wamiliki hawapati fedha zao, wakati abiria wanapokata tiketi, mfumo wa mtandao kuwa chini na maeneo mengine tiketi hazipatikani na changamoto zingine ambazo tumezibainisha,” alisema.

Mhandisi Kisaka aliongeza kuwa changamoto 17 zimefanyiwa kazi na taarifa rasmi wameiwasilisha kwa Naibu Waziri huyo ambapo imejadiliwa na kubainika kwamba kuna umuhimu wa kufanyika maboresho ya kisheria na yapo maeneo mengine yanahitaji kufanyiwa kazi na wadau.

Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa kamati imekubaliana kurudi kufanyia kazi maeneo machache ambayo bado ni changamoto kwa wamiliki wa mabasi kwa lengo la mfumo huo kuanza kutumika Aprili, mwakani.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi