[caption id="attachment_42175" align="aligncenter" width="900"] .Meneja Mkuu wa Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC) Mhandisi akisisitiza jambo wakati akiwasilisha mada mwishoni mwa wiki mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa miradi ya jotoardhi nchini.[/caption]
Na Mwandishi Wetu
Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC) inatarajia kuzalisha megawati 200 za umeme wa jotoardhi na megawati 500 za joto kwa ajili ya matumizi mengineyo ifikapo mwaka 2025.
Akizungumza katika mahojiano maalum na mwandishi wa habari hii, mara baada ya Semina kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Jijini Dodoma hapo jana, Meneja Mkuu wa Kampuni ya hiyo Mhandisi Kato Kabaka alisema kuwa dhamira ya Kampuni hiyo ni kuendeleza miradi ya kipaumbele ili kutimza azma ya uzalishaji uliopangwa kufikia 2025.
Mhandisi Kabaka alisema "Tumejipanga kuendeleza miradi ya vipaumbele ya ngozi, Songwe, Luhoi, Kiejo- Mbaka na Natron ambapo umeme utakaozalishwa utachangia kupunguza gharama za za uwekezaji katika viwanda na maeneo ya uzalishaji."
Akizungumzia baadhi ya miradi ya kimkakati Mhandisi Kabaka alisema kuwa mradi wa Ngozi Mbeya ulioanza mwaka 2015 utakamilika mwaka 2023 ambao upo katika hatua ya uchorongaji wa visima vitatu vya majaribio na ambavyo vinavyotarajiwa kukamilika ndani ya miezi 23 na kuzalisha megawati 30.
Alifafanua kuwa umeme wa Jotoardhi ni wa uhakika na endelevu (stable renewable) na unachangia katika usalama wa nishati (energy security), Jotoardhi ni chanzo kisichoisha na kisichosafirishwa nje ya nchi ikilinganisha na mafuta, mkaa, na gesi.
Mhandisi Kabaka alisema "Gharama za kuzalisha umeme wa jotoardhi ni nafuu ikilinganishwa na nishati zinazozalishwa kupitia vyanzo vingine".
Alibainisha kuwa umeme unaotokana na jotoardhi unaweza kutumika maeneo yasiyofikiwa na gridi ya Taifa kwa sababu za kuwa mbali na gridi hiyo.
Aliongeza kuwa nishati hiyo ina faida nyingi na itachangia kuendeleza sekta muhimu katika uchumi ikiwemo kilimo, ufugaji, utalii,viwanda vidogovidogo na hutumika kama tiba (relaxation and wellness- Balneology).
[caption id="attachment_42176" align="aligncenter" width="713"]Aidha, alitaja baadhi ya mikoa yenye rasilimali jotoardhi nchini Tanzania ambayo ni pamoja na; Arusha, Dodoma, Iringa, Kagera, Katavi, Kilimanjaro, Manyara, Mara, Mbeya, Morogoro, Pwani, Rukwa, Shinyanga, Singida, Songwe na Tanga.
Mikakati mingine ya TGDC ni kujenga uwezo wa wataalamu na kupata vifaa vya msingi na kuweka mazingira wezeshi katika uendelezaji wa Jotoardhi.
Umeme wa Jotoardhi ni rafiki wa mazingira na haichangii hewa ya ukaa hivyo inasaidia katika utunzaji wa mazingira.
Semina kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imefanyika kwa siku mbili Jijini Dodoma mwishoni mwa wiki ikilenga kuwajengea uwezo wajumbe hao katika miradi inayotekelezwa na Taasisi zilizopo chini ya Wizara hiyo ikiwemo TGDC, TPDC, Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) na Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA).
(Picha zote na TGDC)