Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TFRA Yaimarisha Matumizi ya TEHAMA
Mar 19, 2025
TFRA Yaimarisha Matumizi ya TEHAMA
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Bw. Joel Laurent akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 19, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, jijini Dodoma.
Na Mwandishi Wetu

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imeimarisha matumizi ya TEHAMA ambayo yamepunguza muda na gharama za kupata huduma kwa wateja.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo, Bw. Joel Laurent amesema hayo leo Machi 19, 2025 katika Ofisi za Idara ya Habari-MAELEZO jijini Dodoma wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa TFRA katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.

“Kutokana na kuimarishwa kwa mifumo ya TEHAMA, muda wa kupata leseni na vibali vya kuingiza na kusafirisha mbolea nje ya nchi umepungua kutoa siku 14 hadi siku mbili (2),” amefafanua Bw. Laurent.

Ameendelea kusema kuwa, matumizi ya mifumo yamewezesha upatikanaji wa takwimu za uhakika zinazoiwezesha Serikali kuweka mipango ya kuendeleza tasnia ya mbolea na Sekta ya Kilimo kwa ujumla.

“Kupitia Mfumo wa Ruzuku ya Pembejeo za Kilimo (Agricultural Inputs Subsidy System), wakulima wanaendelea kupata  fursa ya kuingizwa kwenye mifumo rasmi ya kifedha kupitia kadi janja na fursa ya kupata hati miliki za mashamba, uwezeshaji wa huduma za kibenki pamoja  na huduma nyigine muhimu,” amesema Bw. Laurent.

Aidha, ametaja vipaumbele vya mamlaka hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kuwa ni pamoja na kuimarisha mifumo ya usambazaji wa mbolea ili kuhakikisha mbolea zinawafikia wakulima kwa wakati na kwa gharama nafuu pamoja na kuimarisha udhibiti wa ubora wa mbolea kwa waingizaji, wazalishaji na wasambazaji.

Vipaumbele vingine ni kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea kwa kushirikiana na halmashauri za wilaya, ili kuongeza matumizi ya mbolea pamoja na kuendelea kuhamasisha wakulima kupima afya ya udongo pamoja na kutumia mbolea zinazozalishwa nchini ili kupunguza utegemezi wa mbolea kutoka nje ifikapo 2030 (Ajenda 10/30).

Mamlaka hiyo pia, inaendelea kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya mbolea nchini ili kupunguza utegemezi wa mbolea kutoka nje ya nchi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi