Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TEWW Yajizatiti Kuendelea Kuwakwamua Wasichana Waliokosa Elimu Katika Mfumo Rasmi
May 23, 2018
Na Msemaji Mkuu

Mkufunzi Mkazi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima  Mkoa wa Dodoma Bw. Habibu Muyula   akisisitiza  kuhusu umuhimu wa mafunzo kwa wasichana waliokosa elimu katika mfumo rasmi kutokana na kupata  ujauzito wakati wa ziara yake katika Wilaya ya Bahi Mkoani Dodoma kukagua maendeleo ya wahitimu wa mafunzo hayo kwa awamu ya kwanza  ambao ni matokeo ya mradi wa kuzuia  mimba za utotoni unatekelezwa na Taasisi hiyo na washirika wa maendeleo.

 Na  Frank  Mvungi

 Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) yaendelea  Kuwawezesha Wasichana waolikosa elimu katika mfumo rasmi na wale waliopata ujauzito katika Wilaya ya Bahi na Kongwa Mkoani Dodoma.

Akizungumza  wakati wa mahojiano maalum  kuhusu kukamilika kwa mafunzo ya awamu  ya kwanza  kwa wasichana hao Mkufunzi Mkazi wa Taasisi hiyo Mkoa wa Dodoma Bw. Habibu Muyula amesema kuwa mradi huo  wa kuzuia mimba za utotoni umepata mafanikio makubwa ambapo wahitimu wake wamejifunza kuzalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo batiki, sabuni na unga wa lishe.

Katika mafunzo hayo wahitimu hao wameweza kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo stadi za maisha kama vile uraia, elimu ya uraia,mazingira,  kujitambua na elimu ya afya.

"Katika mafunzo waliyopata wahitmu hawa wa awamu ya kwanza  takribani 159 katika Wilaya ya Bahi sasa wameanza kuzalisha bidhaa mbalimbali hali itakayosaidia kujikwamua kiuchumi na kuchangia katika kujenga uchumi wa viwanda " Alisisitiza  Muyula

Akifafanua Muyula amesema kuwa  wahitimu wa mafunzo hayo wanapaswa kutumia fursa ya Dodoma kuwa jiji kwa kuzalisha bidhaa zenye ubora ili kuendana na mahitaji ya soko ili waweze kushiriki Kikamilifu katika kuleta maendeleo.

Pia alitoa rai kwa wazazi na jamii kwa ujumla kuwaruhusu wasichana waliokosa elimu katika mfumo rasmi kutokana na mimba za utotoni na sababu mbalimbali kutumia fursa ya kuwepo kwa mradi huo kupata mafunzo kwa kujitokeza na  kujiandikisha ili awamu ya pili ya mradi iweze kuanza.

Kwa upande wake Mmoja wa Walimu wa Mafunzo hayo Bw. Richard Chuma amesema kuwa washiriki wa mafunzo hayo walikuwa na mwamko mkubwa hali iliyochochea  kufanikiwa kwa mafunzo hayo.

Aidha alitoa  wito kwa wazazi na Jamii kwa ujumla kuwarusu wasichana waliokosa elimu katika mfumo rasmi kutokana na mimba za utotoni na sababu mbalimbali kuwasaidia ili waweze kushiriki katika mafunzo hayo ya awamu ya pili inayotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Kwa upande wake  mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo awamu ya kwanza Bi Sophia Kassim amesema kuwa baada ya mafunzo hayo wamepata mabadiliko makubwa na sasa wanajitambua hali inayowawezesha kushiriki katika  kuzalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo batiki, sabuni na unga wa lishe.

Pia alitoa wito kwa wasichana waliokosa elimu katika mfumo rasmi  kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mimba kujitokeza kushiriki katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wasichana hao awamu ya pili itakayoanza hivi karibuni katika Wilaya ya Bahi na Kongwa Mkoani Dodoma unakotekelezwa mradi huo.

Mradi wa kuzuia mimba za utotoni unatekelezwa katika Wilaya ya Bahi na Kongwa Mkoani Dodoma na umeonesha mafanikio makubwa kwa awamu ya kwanza ambapo washiriki zaidi ya 348 wameshanufaika  na mradi huo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi