Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TEHAMA Kuibadili Vikubwa Mahakama Tanzania
Dec 06, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Na Beatrice Lyimo-MAELEZO

Matumizi ya mfumo wa teknolojia ya kisasa (TEHAMA) umesaidia kuboresha huduma za Kimahakama nchini.

Hayo yamesemwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel leo jijini Dar es salaam wakati akizungumza kuhusu mafanikio ya miaka ya 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara ndani ya mahakama.

Prof. Elisante amesema kuwa, kabla na wakati wa uhuru mienendo ya kumbukumbu za Mahakama imekuwa ikichukuliwa kwa maandishi na hivyo kusababisha ucheleweshaji wa utoaji haki na huduma mbalimbali za kimahakama ikiwemo kusafirisha nyaraka.

“Tokea enzi ya Ukoloni mienendo ya kumbukumbu za Mahakama katika ngazi zote imekuwa ikichukuliwa Mahakamani kwa maandishi ya mkono, hali hii imekuwa ikisababisha ucheleweshaji wa utoaji haki, hata hivyo Mahakama imeanza kutumia mifumo ya teknolojia ya kisasa ili kuweza kurahisisha utendaji wa shughuli za kimahakama” amefafanua Prof. Elisante.

Aidha, amesema kuwa kupitia Mfumo huo wa TEHAMA, Mahakama ipo mbioni kupata mfumo wa tafsiri ya lugha ya Kiswahili na lugha nyingine (Hata za asili) ili kuweza kurahisisha huduma za kimahakama kwa uharaka kupitia mfumo wa ‘artificial Intelligence’ (kwa lugha ya kitehama).

Aidha, amesema kuwa, wakati wa Uhuru, Mahakama Kuu ilikuwa na masijala mbili zilizokuwepo Dar es Salaam na Arusha na majaji saba (7) lakini hadi sasa mwaka 2021 idadi ya Majaji wa Mahakama kuu imeongezeka na kufikia Majaji 85 na masjala za Mahakama Kuu zimeongezeka kutoka mbili hadi kufikia masijala 17.

“Hadi Mwaka 2021 Mahakama ina jumla ya watumishi 5,889, Majaji Mahakama ya Rufani 24, Majaji Mahakama kuu 85, Wasajili na Naibu wasajili 41, Mahakimu 1,396 na Watumishi wasio Mahakimu 4,343 (wote wakiwa ni Watanzania)” ameongeza Prof. Elisante.

Kwa upande wa miundombinu, Prof. Elisante amebainisha kuwa, Majengo ya Mahakama katika kipindi cha nyuma yalikuwa duni na sasa yameboreshwa na hivyo kupelekea kuwa na ongezeko la idadi ya Mahakama katika ngazi zote ambapo kwa sasa idadi ya Mahakama Kuu kuna vituo 17, divisheni 4 za Mahakama Kuu, Mahakama za Hakimu Mkazi 29, Mahakama za Wilaya 120 na Mahakama za Mwanzo 960.

Mbali na hayo Prof. Elisante ametoa wito kwa wananchi kutii Sheria bila shuruti, kufuata maelekezo sahihi ya upatikanaji haki (Usijichukulie Sheria Mkononi), kufahamu haki yako na Msaada, pia umuhimu wa kuhimiza mashauriano na maridhiano kuanzia ngazi ya familia na hata taasisi kabla ya kuelekea Mahakamani.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi