Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TBS Yawataka Wajasiriamali Kuthibitisha Ubora wa Bidhaa Zao
Oct 21, 2019
Na Msemaji Mkuu

Na Mwandishi Wetu, Pwani

WAFANYABIASHARA na wajasiriamali mkoani Pwani wametakiwa kujitokeza kwa wingi kwenye ofisi za Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa ajili ya kuthibitisha ubora wa bidhaa wanazozalisha ili kuondokana na vikwazo vya kibiashara ndani na nje ya nchi.

Ushauri huo ulitolewa jana Ofisa Uhusiano wa TBS, Neema Mtemvu, wakati akizungumza washiriki wa Wiki ya Viwanda, Uwekezaji na Biashara mkoani Pwani iliyoanza Oktoba 17, mwaka huu ikitarajiwa kufikia kilele chake Oktoba 23.

Mtemvu, alisema shirika hilo limeshiriki wiki hiyo Viwanda, Uwekezaji na Biashara kwa ajili ya kutoa elimu ya viwango kwa wafanyabiashara na wajasiriamali hasa kuhusiana na umuhimu wa kupata alama ya ubora.

Alisema kwa wajasiriamali gharama za kupata alama za ubora ni bure, kwani tayari zinalipwa na Serikali.

Alifafanua kwamba kinachotakiwa ni wajasiriamali kupata barua ya utambulisho kutoka Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) na kuipeleka TBS, ambapo mchakato wa kuwapatia alama ya ubora unaanza mara moja. Mtemvu, alisema shirika hilo inatambua mchango wa wajasiriamali katika kukuza pato la taifa na kutengeneza ajira kwa wananchi wengi, ndiyo maana kuna mchakato endelevu wa kutoa elimu kwa wajasiriamali kwa kuwa na hilo ni sehemu ya majukumu ya shirika ili waweze kupata alama ya ubora.

Alisema katika kuelekea uchumi wa viwanda ni lazima kuzingatia viwango, ndiyo maana wamekuwa wakishiriki maonesho mbalimbali ikiwemo wiki ya Viwanda, Uwekezaji na Biashara mkoani Pwani kwa ajili ya kutoa elimu.

Mtemvu alitoa wito kwa wajasiriamali akisema suala la wao kukidhi matakwa ya viwango vya kitaifa kwa bidhaa wanazozalisha na zinazosindikwa ni la msingi kwa kuwa ndiyo njia pekee ya kupanua wigo wa masoko ya bidhaa zao ndani na nje ya nchi.

"Kwa hiyo uwepo wetu hapa ni fursa muhimu ambayo inamlenga kumwinua mzalishaji aweza kushindana na kuuza bidhaa zake bila woga," alisema Mtemvu.

Alitoa mwito kwa wananchi wa Pwani na nchini kote kwa ujumla kuhakikisha wanatumia bidhaa zenye ubora.

Wakati huo huo, Mtemvu alisema wiki hiyo ya Viwanda, Uwekezaji na Biashara wameitumia kama fursa kuwapa taarifa washiriki kuwa baadhi ya majukumu yaliyokuwa yakitekelezwa na iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) ya chakula na vipodozi sasa hivi yamehamia TBS.

"Serikali ya Awamu ya Tano imeliona hilo na kwa hatua hiyo sasa inakuwa ni rahisi mno kupata alama ya ubora, kwani ukishapata alama ya ubora utaweza kufanya biashara na vile vile ule mzunguko uliokuwepo awali wa kuzunguka wa kwenda TFDA halafu urudi TBS utakuwa umepungua," alisema Mtemvu

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi