Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TBS Yatoa Mafunzo kwa Wadau wa Mafuta Zaidi ya 1,700
Oct 02, 2020
Na Msemaji Mkuu


Na Mwandishi Wetu 

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limetekeleza mpango wa mafunzo kwa wazalishaji, wasambazaji na wauzaji wa mafuta ya kula zaidi ya 1,700 kwa kuwaelimisha kuhusu uzalishaji bora, uhifadhi na ufungashaji sahihi wa bidhaa za mafuta pamoja na umuhimu wa kuzingatia na kuweka taarifa sahihi na muhimu kwenye vifungashio.

Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora TBS, Lazaro Msasalaga, alisema mafunzo hayo yamelenga kuwajulisha wadau wa mafuta ya kula fursa zilizopo ndani ya Serikali ili kuwawezesha kuboresha bidhaa zao ili ziweze kukidhi matakwa ya viwango na hatimaye kupananua wigo wa soko la ndani na nje ya nchi na  kuongeza uzalishaji utakaopelekea kuinua uchumi wao.


"Nawashauri wadau kuzingatia kanuni za uzalishaji na uhifadhi bora na salama ili kuepuka kupoteza masoko na kero ya kukutwa na bidhaa hafifu ambazo zitawalazimu kuteketeza gharama zao," alisema Msasalaga.

Kwa upande wake Meneja wa Utafiti na Mafunzo TBS, Hamis Sudi Mwanasala, alisema mafunzo hayo kwa wadau wa sekta ya mafuta ya kula yataendeshwa katika mikoa yote nchini na kwa kuanzia yameendeshwa katika Kanda ya Kati ikijumuisha mikoa ya Dodoma, Singida na Tabora.


Nae Kaimu Mkuu wa Kanda ya Kati TBS, Salome Emmanuel aliwasisitiza wajasiriamali ambao bado bidhaa zao za mafuta hazijapatiwa nembo ya ubora, kuchangamkia fursa ya bure kwa kutuma maombi ya kutumia alama ya ubora kupitia SIDO ili Serikali iwatambue kama wajasiriamali wadogo na kati na waweze kuhudumiwa bure kwa kuwa bidhaa ya mafuta inaangukia katika kiwango cha lazima, hivyo kulazimika kukidhi matakwa ya viwango kwa mujibu wa sheria.


Bi. Salome aliongeza kuwa lengo ni kuwaelimisha madhara yanayotokea pindi mafuta yanapoanikwa juani kwani mwanga, joto na hewa hupelekea mafuta kuharibika kabla ya muda wa mwisho wa matumizi na kusababisha madhara ya kiafya.

Mzalishaji wa Mafuta ya kula, Daud Makala na Muuzaji wa Mafuta hayo, Eunice Maneno walioshiriki mafunzo hayo katika jijini Dodoma, walipongeza juhudi zinazofanywa na TBS kwa  kuhakikisha wanawasaidia wadau wa sekta mbalimbali hususani mafuta ya kula kwa kuzingatia viwango ili kuweza kupata masoko ndani na nje ya nchi na kuwa na ushindani huru sokoni.


Nao wauza mafuta ya kula katika Soko Kuu la Singida na Tabora, wameiomba Serikali kurahisisha upatikanaji wa vifungashio na kuhakikisha vinauzwa kwa bei nafuu ili hata wajasiriamali nchini waweze kupaki mafuta yao kwa vifungashio bora na salama 
TBS imetoa mafunzo hayo kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara, Shirika la Viwanda Vigogo Vigogo (SIDO), maOfisa biashara, afya na maendeleo wa wilaya.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi