Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TBS Yakusanya Bilioni 3.9 Katika Zoezi la Ukaguzi wa Magari Bandarini Yanayotoka Nje kwa Mwezi Aprili Mpaka Agosti
Aug 06, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo amesema Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limekusanya takribani Shilingi Bilioni 3.9 katika zoezi la ukaguzi wa magari bandarini yanayotoka nje ya nchi katika kipindi cha mwezi Aprili hadi Agosti 03, 2021 na kuokoa kiasi cha shilingi Bilioni 2.7 ambayo kwa utaratibu wa zamani, TBS kwa niaba ya Serikali tungepata asilimia 30 pekee ya fedha hizi na asilimia 70 ingebaki nje ya nchi.

Prof. Mkumbo ameeleza hayo leo Agosti 05, 2021 wakati alipoambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah kutembelea Bandari kuu ya Dar es salaam kwenye kitengo cha ukaguzi wa magari yanayoingizwa nchini unaofanywa na TBS na kujionea shughuli zinavyoendelea.

Aidha, Prof Mkumbo amesema TBS inaendelea kuboresha zoezi na utaratibu wa ukaguzi wa magari yanayoingizwa hapa nchini ambapo mpaka agosti 03, 2021 yamekaguliwa magari 11,079, kati ya m hayo 7,700 yalikidhi ubora na magari yaliyobaki yalikwenda kutengenezwa na kati yake magari 1,890 yaliweza kukidhi ubora baada ya matengenezo na mengine yaliyobaki yapo gereji yakiendelea kurekebishwa.

 “Kwa kuamua kutekeleza mpango huu, Serikali inaokoa fedha nyingi ambazo zingebaki nje hivyo kwa kipindi cha miezi minne tumekusanya takribani Bilioni 3.9 na fedha hii inaingia katika mfuko mkuu wa Serikali”. Amesema Prof.Mkumbo.

Pamoja na haya Prof. Kitila Mkumbo ametoa wito kwa wananchi wanaoagiza magari na wafanyabishara wanaofanya biashara hiyo kuendelea kuunga mkono utaratibu huo mzuri na kutoa ushirikiano kwa TBS na pale ambapo kuna upungufu waendelee kutoa maoni kama ambavyo wamekuwa wakifanya na Serikali kupitia TBS iweze kuyafanyia kazi, wakati huo huo ameipongeza TBS na wafanyakazi wote kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya hapo bandarini.

“Mapema mwaka huu Serikali ilianzisha utaratibu wa kukagua magari yote yanayoingizwa nchini yakaguliwe hapa na TBS ndio iliyokabidhiwa majukumu hayo, leo nimepata nafasi ya kukagua na kujionea kazi inavyoendelea katika vituo vyetu viwili na nimefurahi kuona zoezi hili linaendelea kuimarika” ameleza Waziri Prof. Kitila Mkumbo.

Kwa upande wake, Meneja wa Ukaguzi wa Bidhaa kutoka Nje ya Nchi kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mhandisi Said Mkwakwa amesema, lengo la ukaguzi wa magari yaingiayo nchini unaofanywa na TBS ni kuhakikisha magari yote yaliyotumika yanakaguliwa ili kubaini ubora wake na kazi hiyo waliianza tangu tarehe 15 Aprili, mwaka huu.

Kuanzia tarehe 01 Machi, 2021, utaratibu wa kukagua magari kutoka nje ya nchi ulianza kufanyika baada ya magari hayo kuwasili nchini (Destination Inspection) ambapo waagizaji wote walitakiwa kupeleka maombi TBS na si kwa mawakala kama ilivyokuwa hapo awali.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi