Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TBS Yafanya Msako wa Mifuko Mbadala Tandika
Jan 19, 2020
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_50258" align="aligncenter" width="960"] Maafisa wa Shirika la Viwango Tanzania wakitoa elimu na kufanya ukaguzi wa mifuko mbadala Tandika mwishoni.[/caption]

Na Mwandishi Wetu

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limeendelea kufanya ukaguzi wa kushtukiza kwa wazalisha wakubwa, wa kati na wadogo na wauzaji wa mifuko mbadala ili kuhakikisha mifuko iliyoruhusiwa, ndiyo inayoendelea kuzalishwa na kuingizwa sokoni.

Katika mwendelezo wa ukaguzi huo wa kushtukiza mwishoni mwa wiki maofisa wa shirika hilo walifanya ukaguzi kwenye maduka yaliyopo kwenye soko la Tandika, wilayani Temeke jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari Mkaguzi wa TBS, Lucas Bwila, alisema ukaguzi huo utafanyika nchi nzima ili kujiridhisha kama mifuko iliyoruhusiwa na shirika hilo, ndiyo inayoendelea kuzalisha na kuingizwa sokoni.

"Tupo katika zoezi la kuangalia ubora wa mifuko mbadala ambayo iko sokoni na vile vile kuangalia kama mifuko iliyokwisha katazwa kama bado ipo sokoni," alisema Bwila.

Alisema zoezi hilo limehusisha Wilaya ya Temeke na Kigamboni, jijini Dar es salaam na kwamba ni endelevu kwa nchi nzima.

"Tutapita kila sehemu, tutapita kwa wazalishaji wa mifuko, kwa wauzaji wakubwa, tutapita na kwa wazalishaji wadogo ili kuweza kubaini kama mifuko iliyoruhusiwa ndiyo inaendelea kuuzwa na tunatoa elimu pia," alisema na kuongeza;

"Kwa wauzaji wadogo kama hawa lengo letu kubwa ni kuwapa elimu, kwani wakielewa mifuko wanayotakiwa kuuza iwe na viwango vya aina gani tunaamini moja kwa moja hata mzalishaji hatapata sehemu ya kuuza."

[caption id="attachment_50260" align="aligncenter" width="960"] Maafisa wa Shirika la Viwango Tanzania wakitoa elimu na kufanya ukaguzi wa mifuko mbadala Tandika mwishoni.[/caption]

Bwila, alisema hilo ndiyo lengo la maofisa wa shirika hilo kupita kwa wazalishaji wakubwa, wadogo na wa kati na wauzaji kwa lengo la kuwapa elimu.

Kuhusu walichobaini kwenye ukaguzi wao, Bwila alisema katika zoezi hilo kiuhalisia mafanikio ni makubwa. "Tulipofanya zoezi hili kwa wazalishaji wengi, karibu wote tulipopita tulikuta wanaweka vitu ambavyo ni vya lazima katika matakwa ya kiwango, wanaandika na baadhi ya sampuli ambazo tumechukua nyingi zimefaulu katika maabara zetu," alisema.

Hata hivyo alisema bado kuna changamoto ya kuwepo baadhi ya mifuko michache ambayo haijakidhi viwango na wengi wanawaambia hiyo mifuko mingi ni ya zamani.

Alisema mifuko ambayo imethibitishwa na shirika hilo ina vitu ambavyo lazima mzalishaji avionesha. "Lazima huyo mzalishaji aonesha mifuko hiyo ni ya kupakia nini, huo mfuko uwe umeandikwa, mfuko kuandikwa unapaki kilo nne au kilo tano siyo matakwa halisi ya kiwango," alisema.

Gwila alizidi kufafanua kwamba kisheria ili mfuko uruhusiwe kutumika kuna matakwa ya viwango unatakiwa uwe umekidhi, hivyo alitoa wito kwa wafanyabiashara na wanaozalisha wa mifuko hiyo, wasiendeleze hiyo biashara kwa sababu wakikamatwa watashtakiwa kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande wake muuzaji wa mifuko hiyo, Khalfan Mlapala, alipongeza hatua ya maofisa wa shirika hilo kufanya ukaguzi huo na alitoa wito kwa Serikali kuhakikisha mifuko isiyokithi viwango uzalishaji wake unathibitiwa viwandani ili kuwaepusha kupata hasara.

Alisema pindi mifuko hiyo inapoingia sokoni na baadaye ikagundulika haikidhi viwango wao ndiyo wanaopata hasara. Hata hivyo, alisema elimu inayotolewa na maofisa wa shirika hilo itawasaidia kutambua mifuko isiyotakiwa, hivyo na wao hawataweza kuinunua.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi