Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TASAC Yaanza Kutekeleza Maagizo ya Rais Samia kwa Vitendo
Oct 19, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Mwandishi Wetu - Kigoma

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limesema kuwa limejipanga kutekeleza kwa vitendo agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuufanya Mkoa wa Kigoma kuwa kitovu cha biashara kwa mikoa ya magharibi na nchi za maziwa makuu kwa kuhakikisha wanasimamia kwa tija kubwa vyombo vya usafirishaji majini kwenye ziwa Tanganyika.

Hayo yalisemwa  leo na Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Kaimu Abdul Mkeyenge wakati akizungumza na Waandishi wa Habari mjini Kigoma ambapo alisema kuwa mkoa huo unayo tija kubwa ya kufanya biashara na shughuli za kiuchumi na nchi za maziwa makuu ambapo ziwa Tanganyika kwa sasa ndiyo njia kuu inayohudumia usafirishaji wa bidhaa na abiria kutokana na kuingia kwenye nchi hizo.

Kutokana na hali hiyo, alisema kuwa TASAC imejipanga kuongeza maradufu watendaji wake mkoani Kigoma kuhakikisha shughuli zinazohusiana na taasisi hiyo na wasafirishaji majini zinashughulikiwa kwa urahisi kwa kipindi kifupi ili kusiwe na mkwamo kwenye utekelezaji wa shughuli za biashara na uchumi.

Mkeyenge alisema kuwa wamejipanga pia kuhakikisha taratibu za kisheria za kimataifa na zile za Tanzania za  usalama wa usafirishaji majini ziwa Tanganyika kwa vyombo vinavyokwenda nchi za Burundi,Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Zambia zinatekelezwa kikamilifu.

“Zipo changamoto za usimamizi wa taratibu na sheria kwa wenzenu wa nchi zinazozunguka ziwa Tanganyika ikiwemo meli na boti za abiria kuchanganya bidhaa hizo wakati sheria za Tanzania zinakataza bidhaa hizo mbili kuchanganywa, hivyo vipo vikao na majadiliano yanaendelea ili kuliweka jambo hilo sawa", Alisema Mkeyenge.

Akizungumzia mpango wa Serikali wa kuufanya Mkoa Kigoma kuwa kitovu cha biashara, Mwenyekiti wa Chama cha Wasafirishaji wa maboti mkoani Kigoma, Ibrahim Sendwe alisema kuwa jambo hilo ni muhimu na litachochea biashara na uchumi wa mkoa huo.

Sendwe alisema kuwa wao kama wasafirishaji wa mizigo na abiria wako tayari kushiriki kwenye mipango hiyo lakini wanapaswa kupewa uelewa wa fursa ambazo kwao wanaweza kuzitumia kuleta tija kwenye mpango huo.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa wamejipanga kuhakikisha wanasimamia taratibu za usalama wa usafirishaji abiria ikiwemo taratibu na sheria za usafirishaji wa abiria na mizigo ili shughuli zao zisipingane na maelekezo ya Serikali.

Kwa upande wake Mmiliki wa boti zinazofanya shughuli zake ziwa Tanganyika, Almas Juma amemshukuru Rais Samia kwa maboresho makubwa yanayofanywa kwenye bandari ya Kibirizi na miradi mikubwa kwa mkoa Kigoma kwenye sekta ya biashara na uchumi kwani imechochea shughuli za biashara na uchumi mkoani humo.

Hata hivyo Juma ameomba Serikali ya Rais Samia kuondoa tozo ya Viza inayotozwa kwa wasafiri wanaoingia mkoani Kigoma kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na ada ya Dola za Marekani 20 kwa wafanyabiashara wadogo ambao hawana nyaraka za kufanya biashara.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi