Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema Tanzania imefanikiwa kuzuia tani 216 sawa na asilimia 86 ya uzalishaji wa kemikali hatari kwa tabaka la ozoni ambazo zingeingia nchini na kuleta madhara.
Amesema mafanikio hayo yamekuja kutokana na Tanzania kuungana na nchi zingine duniani kuridhia na kusaini Itifaki ya Montreal mwaka 1987 ambayo imechangia katika hifadhi ya tabaka la ozoni.
Dkt. Kijaji amesema hayo wakati akizungumza katika kipindi cha ‘Mazingira Yetu na Tanzania Ijayo’ kinachotayarishwa na Ofisi ya Makamu wa Rais na kurushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Septemba 16, 2024.
Amesema Itifaki hiyo pia imekuwa ni nyenzo muhimu katika kuchangia
jitihada za kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi yanayochangia joto duniani.
“Kabla ya kuridhiwa kwa itifaki hii tabaka letu la ozoni lilianza kuathirika na baada ya kuanza kutekeleza shughuli zilizomo kwenye itifaki hii iliyoridhiwa na nchi 197, tayari tumesharejesha asilimia 98 ya tabaka la ozoni na tumeshazuia tani milioni moja nukta nane ambazo zingeingia duniani, kwenye viwanda vyetu, kwenye shughuli za binadamu zingeendelea kumong’onyoa tabaka na dunia yetu ingekuwa kwenye hatari kubwa,” ameeleza.
Kuhusu jitihada za Tanzania kukabiliana na uharibifu wa tabaka la ozoni, Dkt. Kijaji amebainisha kuwa mwaka 2007 Serikali iliandaa kanuni za kuzuia uingizaji wa kemikali hatarishi kwa tabaka hilo na kuzifanyia maboresho mwaka 2022 ili ziendane na wakati.
Halikadhalika, amesema kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imekuwa ikitoa elimu kwa maafisa katika mipaka ya nchi, bandari, forodha na viwanja vya ndege ili wazitambue kemikali hizo na wasaidie kuzuia.
Amesema mkakati wa Serikali ni kuhakikisha mwaka 2030 hatuhitaji kuwa na kemikali za aina hii ambapo elimu hutolewa kwa mafundi mchundo wa viyoyozi, majokofu wanapotengeneza waweze kuzuia zisiende hewani na kuharibu tabaka la ozoni.
Hivyo, Waziri Dkt. Kijaji ametoa wito kwa wananchi kulinda tabaka la ozoni na kwamba endapo litaharibiwa dunia nayo itakuwa imeharibiwa na kuruhusu mionzi ya jua kufika kwenye uso wa dunia na kusababisha magonjwa.
ya saratani ya ngozi, mtoto wa jicho, upungufu wa kinga dhidi ya maradhi na kujikunja kwa ngozi.
Itakumbukwa Septemba 16, 2024 Tanzania iliungana na nchi zingine kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni ambayo kaulimbiu kwa mwaka huu ni ‘Itifaki ya Montreal: Kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi’.