Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tanzania Yapewa Tuzo ya Kimataifa ya Kupambana na Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza
Sep 28, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na Fatma Salum

Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imepata Tuzo ya Kimataifa ya Kupambana na Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (NCDs) kwenye mkutano wa Viongozi wa Juu wa Umoja wa Mataifa (United Nations High Level Meeting on NCDs) unaoendelea mjini New York nchini Marekani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wizara hiyo, Waziri Ummy Mwalimu alipokea tuzo hiyo jana tarehe 27 Septemba, 2018 kutoka kwa Kikosi Kazi Maalum cha Umoja wa Mataifa cha Kupambana na Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (UN Interagency Task Force on the Prevention & Control of NCDs- UNIATF).

Taarifa hiyo inaeleza kuwa tuzo hiyo imetokana na juhudi za Wizara ya Afya za kupambana dhidi ya Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (NCDs), hususan kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kufanya mazoezi ya mwili mara kwa mara.

Aidha Waziri Ummy amelishukuru Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza la Tanzania (TANCDA) ambao waliandika andiko la kuitambulisha dunia kuhusu juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza na dunia ikaona umuhimu wa juhudi hizo.

“Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (NCD) ndiyo yanayoongoza duniani kwa sasa kwa kusababisha ulemavu na vifo vingi.  Nchini Tanzania asilimia 34 ya vifo vilivyorekodiwa hospitali mwaka 2017 vimesababishwa na magonjwa haya, isitoshe kupambana na NCD ni miongoni mwa mikakakati ya Mpango wa Kimataifa wa Maendeleo Endelevu (SDG) ya kupunguza kwa theluthi moja vifo vya mapema vitokanavyo na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ifikapo mwaka 2030,” alisema Waziri Ummy.

Pia alibainisha kuwa Serikali kwa kushirikiana na TANCDA pamoja na wadau wengine inaamini kwamba afya za wananchi zitaendelea kuboreshwa kwa kuweka mikakati madhubuti, kuzingatia utekelezaji wa sera mbalimbali za afya na kuhakikisha Watanzania wanapata elimu sahihi ya kujikinga na kuyadhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Magonjwa yasiyo ya kuambukiza ni magonjwa sugu au ya muda mrefu, ambayo hayawezi kuambukizwa kwa maana kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine. Magonjwa hayo yapo mengi kama vile Kisukari, Saratani, Shinikizo la Damu na Mishipa ya Fahamu, Magonjwa Sugu ya Mfumo wa Hewa, Magonjwa Sugu ya Figo, Macho na Meno, Selimundu (sikoseli) na mengineyo.

Tanzania ni miongoni mwa nchi 9 duniani ambazo zimefanikiwa kupata tuzo hiyo ambayo imetolewa kwa mara ya kwanza katika ngazi ya kiserikali.

   

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi