Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tanzania yafanikiwa kudhibiti mfumuko wa bei Afrika Mashariki
Jun 08, 2017
Na Msemaji Mkuu

Benny Mwaipaja-WFM, Dodoma

Pamoja na malalamiko na manung’uniko ya hali ngumu ya maisha kwa watanzania wengi, Tanzania ndio yenye kiwango cha chini cha mfumuko wa bei wa wastani wa asilimia 6.1 kwa mwezi Mei 2017 kwa nchi za Afrika Mashariki.

Hayo yamebainishwa leo bungeni Mjini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango akiwasilisha Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2017/18.

Mhe. Dkt. Mpango amesema mfumuko wa bei katika nchi za Afrika Mashariki kwa mwaka 2016 uliendelea kuwa wa kiwango cha tarakimu moja, ambapo Rwanda ilikuwa na asilimia 7.1, Uganda asilimia 5.4, Tanzania asilimia 5.2, Kenya asilimia 6.3 na Burundi asilimia 5.6.

Alisema kufikia mwezi Aprili 2017, mfumuko wa bei kwa nchi hizi ulipanda, ambapo kwa Burundi ulifikia asilimia 21.10, Rwanda asilimia 13.0; Kenya asilimia 10.28; Uganda asilimia 6.4 na Tanzania asilimia 6.4.

“Hata hivyo, kwa upande wa Tanzania mfumuko wa bei umeendelea kushuka mpaka asilimia 6.1 kwa mwei Mei 2017” amesema Dkt. Mpango

Mhe. Dkt Mpango amesema kwa  miaka minne mfululizo, wastani wa mfumuko wa bei kwa Tanzania umeendelea kupungua, ukibaki katika kiwango cha tarakimu moja.

Amesema kwa mwaka 2016, mfumuko wa bei ulifikia wastani wa asilimia 5.2 ikilinganishwa na asilimia 5.6 mwaka 2015. Kupungua kwa wastani wa mfumuko wa bei nchini kulichangiwa kwa kiasi kikubwa na: mwenendo wa kushuka kwa bei za mafuta ya petroli katika soko la dunia na nchini; kuimarika kwa upatikanaji wa vyakula nchini na hivyo kuimarisha wastani wa bei; na kuwepo kwa sera madhubuti za usimamizi wa bajeti na fedha.

Mhe. Dkt. Mpango amesema mfumuko wa bei uliongezeka kidogo, ambapo ulifikia asilimia 6.4 mwezi Aprili 2017 lakini ukiwa ndani ya maoteo ya wastani wa tarakimu moja (asilimia 5 – 8) kwa mwaka 2017.

Hali ya kuongezeka kwa mfumuko wa bei nchini ilichangiwa na hofu iliyotokana na kuchelewa kwa msimu wa mvua katika maeneo mengi nchini na hivyo kuwepo kwa taharuki ya kutokea upungufu wa chakula. Hata hivyo, maeneo mengi yamepata mvua ya kutosha na hivyo bei  ya chakula nchini inatarajiwa kupungua.

Mhe. Dkt. Mpango amesema kasi ya ukuaji wa uchumi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ilishuka kutoka wastani wa asilimia 6.5 mwaka 2015 hadi asilimia 5.3 mwaka 2016 ijapokuwa Jumuiya hii iliendelea kuongoza kwa ukuaji miongoni mwa Jumuiya mbalimbali za Afrika.

Amesema kasi ndogo ya ukuaji wa uchumi katika Jumuiya hii ilichangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo kushuka kwa bei za bidhaa na kudorora kwa uchumi wa dunia. Maoteo ya mwenendo wa uchumi katika ukanda huu yanaonesha utakua kwa wastani wa asilimia 5.7 mwaka 2017 na asilimia 6.0 mwaka 2018.

“Matarajio haya yanazingatia hatua zinazochukuliwa na nchi za ukanda huu katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na uendeshaji biashara kama vile kuwa na maeneo tengefu ya ujenzi wa viwanda (industrial parks), hususan, vya nguo, bidhaa za ngozi, kilimo, madawa na vifaa tiba” ameongeza Dkt. Dkt. Mpango

Amesema kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), kasi ya ukuaji wa uchumi ilishuka kutoka wastani wa asilimia 1.9 mwaka 2015 hadi asilimia 1.1 mwaka 2016.

Mhe. Dkt. Mpango amesema kasi ndogo ya ukuaji wa uchumi katika Jumuiya hii ilichangiwa na uhaba wa nishati ya umeme pamoja na ukame uliochangiwa na mabadiliko ya hali ya hewa ya La Nina.

Amesema licha ya kasi ndogo ya ukuaji, Jumuiya hii iliendelea kuwa ya tatu kwa ukuaji miongoni mwa Jumuiya za barani Afrika na unatarajiwa kukua kwa wastani wa asilimia 1.4 mwaka 2017.

Waziri wa Fedha amesema mfumuko wa bei ulifikia asilimia 10.5 mwaka 2016 ikilinganishwa na asilimia 5.7 mwaka 2015, ukichangiwa na ukame na kuyumba kwa utekelezaji wa sera za mapato na matumizi kwa baadhi ya nchi wanachama.

Ameeleza kuwa matarajio katika nchi hizo ni kuwa kwa mwaka 2017 mfumuko wa bei utapungua hadi kufikia asilimia 8.7 kutokana na kushuka kwa gharama za bidhaa, kuimarika kwa upatikanaji wa nishati ya umeme, na uthabiti wa bei ya mafuta; na kuimarika kwa hali ya hewa.

     

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi