Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tanzania Yaandika Historia Majaribio Treni ya Umeme
Feb 26, 2024
Tanzania Yaandika Historia Majaribio Treni ya Umeme
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Mobhare Matinyi akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu safari ya majaribio ya treni kupitia reli ya kisasa
Na Mwandishi Wetu - Maelezo

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Mobhare Matinyi, amesema Tanzania imeandika historia nyingine kwa kuanza kwa majaribio ya treni ya umeme kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro na kurudi Dar es Salaam.

Matinyi amesema hayo leo Februari 26, 2024, wakati akihojiwa na Waandishi wa Habari kwenye safari hiyo ya majaribio ambapo treni hiyo ikiwa na abiria zaidi ya 200 imetumia takriban saa mbili na dakika ishirini kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita iliahidi kutekeleza mradi huo, ambapo leo TRC imefanya majaribio kwa mara ya kwanza kwa treni hiyo ya umeme ikiwa na abiria ili kuangalia ufanisi wa kichwa cha treni na mabehewa kabla ya kuanza rasmi kwa shughuli za usafirishaji.

“TRC wamefanya majaribio ya safari ya treni kutoka Dar es salaam hadi Morogoro na kurudi Dar es salaam ikiwa ni ukamilishaji wa ahadi ya Mhe. Rais Samia kwa watanzania kuhusu usafiri huo wa treni ya umeme. Mafanikio ya serikali hii ni mengi, kuna afya, barabara, maji na sekta nyingine zinazoendelea kuboreshwa kila kukicha,” amesema Bw. Matinyi.

Ameendelea kusema kuwa wanapaswa kujivunia nchi yao, kwani ubora wa treni hiyo hauna tofauti na zile za nchi zilizoendelea, hivyo wafanyabiashara na watanzania kwa ujumla wajiandae kutumia fursa hiyo vizuri hasa kwa kupunguza muda wa safari.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi