Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tanzania, Uganda Kuendeleza Ushirikiano Miradi ya Kimkakati
Oct 10, 2023
Tanzania, Uganda Kuendeleza Ushirikiano Miradi ya Kimkakati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akizungumza wakati akiwasilisha salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Maadhimisho ya Miaka 61 ya Uhuru wa Nchi ya Uganda yaliyofanyika Oktoba 9, 2023 kwenye Viwanja vya Kitgum kaskazini mwa nchi ya Uganda.
Na Neema Mbuja, KAMPALA

Serikali ya Tanzania imeahidi kuendeleza Ushirikiano, Umoja na Mshikamano na nchi ya Uganda kwa manufaa ya nchi zote mbili.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko wakati akiwasilisha salamu za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Maadhimisho ya Miaka 61 ya Uhuru wa Nchi ya Uganda yaliyofanyika Oktoba 9, 2023 kwenye Viwanja vya Kitgum kaskazini mwa nchi ya Uganda.

Akitoa salamu hizo kwa niaba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Biteko alisema kuwa Mheshimiwa Rais anathamini mchango na maendeleo yaliyofikiwa na nchi ya Uganda  katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kiuchumi.

"Mhe Rais anakupongeza Sana kwa siku hii muhimu ya miaka 61 ya Uhuru na wananchi wote wa Uganda na ameahidi kuendelea kushirikiana katika kujenga uchumi wa nchi hizi mbili  na Afrika Mashariki kwa ujumla.

Aidha, Mhe Rais alimshukuru Mhe Rais Yoweri Kaguta Museveni kwa jitihada zake za kudumisha umoja na mshikamano kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Tanzania na Uganda zimekuwa na mahusiano na ushirikiano wa muda mrefu kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kiuchumi ikiwemo utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima Uganda mpaka Tanga, pamoja na miradi mbalimbali kwenye sekta ya Nishati, Utalii, Kilimo,

Historia ya nchi hizi mbili ilianza tangu kipindi cha harakati za Uhuru baina ya waasisi wa nchi hizi mbili na ushirikiano huu unaendelezwa na kudumishwa kwa  umoja, amani, mshikamano na utu uliopo baina ya nchi hizi mbili

Hafla ya Miaka 61 ya Uhuru wa Uganda ilihudhuriwa na Makamu wa Rais Burundi Mhe. Prosper Bazombanza, Wawakilishi kutoka Jumuiya ya Falme za kiarabu, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka Kenya Peter Mathuki, Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao nchini Uganda, Mawaziri, wabunge kutoka nchini Uganda na wananchi wa nchi hiyo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi