Julai 07 kila mwaka ni Siku ya Kiswahili duniani, siku iliyopendekezwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) mwaka 2022, ikiwa ni kuitambua lugha ya Kiswahili kama alama muhimu ya muafrika, yenye wazungumzaji zaidi ya milioni 350 duniani kote.
Barani Afrika, lugha ya Kiswahili ni utambulisho wa muafrika, ambapo Mwaka 2019, lugha ya Kiswahili ilitambuliwa na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kuwa lugha pekee ya Kiafrika.
Baadhi ya nchi barani Afrika ikiwemo Afrika Kusini, Botswana, Ghana na Ethiopia tayari zimeanza kufundisha lugha ya Kiswahili Shuleni ikiwa ni jitihada za kuliunganisha Bara la Afrika, wazo ambalo lilikuwa la baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika miaka ya 1960.
Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendeleza maono hayo pamoja na kuja na mikakati kadha wa kadha ya kukuza lugha hii adhimu, ikiwemo dhana maarufu ya ‘Kuibidhaisha lugha ya Kiswahili’, dhana inayosisitiza kukuza na kukiuza Kiswahili kama bidhaa nje ya mipaka ya Tanzania.
Julai 6, 2023 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akizungumza katika ufunguzi wa maadhimisho ya siku ya Kiswahili duniani, aliziagiza wizara zenye dhamana ya lugha ya Kiswahili kusimamia kikamilifu mkakakti wa kukuza na kubidhaisha lugha ya Kiswahili ndani na nje ya Tanzania.
“Andaeni nafasi za Watanzania kufundisha Kiswahili katika nchi mbalimbali duniani, kila mmoja awajibike kuhakikisha Kiswahilli kinakua na kuendelezwa” alisema Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa.
Pamoja na mikakati mbalimbali ya kukuza lugha ya Kiswaili, Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuweka mazingira mazuri ya kuikuza zaidi lugha ya Kiswahili duniani ambapo Moja ya mkakati ni kuanzishwa kwa Kongamano la Kimataifa la Kiswahili.
Kongamano hili ni nyenzo muhimu katika kukuza lugha ya Kiswahili kwa sababu kwa mara ya kwanza, tangu Tanzania ipate uhuru, Serikali imefanya kongamano la kwanza la lugha ya Kiswahili jijini Havana, nchini Kuba ikiwa ni hatua ya kwanza ya kuipeleka lugha hii adhimu ya Kiswahiili duniani.
Akizungumza katika ufunguzi wa kongamano hilo Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, alifafanua sababu za kufanya kongamano hili nchini Kuba.
“Tanzania ilikuwa kituo muhimu cha wapigania uhuru wa Bara la Afrika, na lugha kuu iliyotumika wakati wa harakati hizo ilikuwa ni Kiswahili. Tunapoendelea na mapambano ya kuleta ukombozi wa kiuchumi katika Bara la Afrika na ambapo tungependa kushirikiana zaidi na wenzetu wa Ukanda wa Karibe, tunaamini Kiswahili kitarahisisha na kuwezesha Mawasiliano kwa ajili ya mtangamano, biashara, utalii na uwekezaji barani Afrika”.
Kadhalika, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo amewasisitiza watanzania kuchangamkia fursa zilizopo wakati lugha ya Kiswahili inaendelea kukuwa na kuenea zaidi katika maeneo mbalimbali duniani.
“Kiswahili kwa sasa kinazungumzwa na takriban watu milioni 350 duniani na wazungumzaji wanaendelea kuongezeka. Ni muhimu kuibeba bendera hii vizuri” alisisitiza Mhe. Balozi Kombo.
Pamoja na mambo mengine, uzinduzi wa kongamano hilo la kwanza la kimataifa la Kiswahili nchini Kuba, umeambatana na uzinduzi rasmi wa Kamusi ya Kihispania kwenda Kiswahili, Kitabu cha maneno na misemo ya kila siku kati ya Kiswahili na Kihispania pamoja na uzinduzi wa sanamu ya Baba Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ikiwa ni ishara ya uhusiano wa kihistoria uliyopo kati ya Tanzania na Kuba uliyoasisiwa na viongozi wa kwanza wa mataifa hayo, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Fidel Castro wa Kuba.