Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tanzania Nchi ya Tano Ulimwenguni Uzalishaji wa Korosho
Oct 08, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO

Nchi ya Tanzania imetajwa kuwa nchi ya tano Duniani kwa uzalishaji wa korosho kati ya nchi 46 zinazolima zao hilo ikiongozwa na nchi za IvoryCoast, India, Vietnam na Cambodia ambapo kwa Afrika Tanzania inafuatiwa na nchi ya Nigeria.

Takwimu hizo zimetajwa leo jijini Dodoma na Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania, Francis Alfred wakati akiongea na Waandishi wa Habari kuhusu shughuli mbalimbali za bodi hiyo kwa mwaka 2021/2022 na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka 2022/2023.

Kaimu Mkurugenzi Alfred amesema kuwa Serikali imejipanga kuongeza juhudi za uzalishaji kwa kuwapa wakulima nyenzo mbalimbali na kuendelea kushirikiana na wadau wote katika mnyororo wa zao hilo ili kuhakikisha mkulima anazalisha na kuuza korosho zake kwa tija kwa maendeleo ya tasnia ya korosho nchini.

“Katika juhudi za kuongeza uzalishaji wa korosho, tumejikita zaidi katika mashamba makubwa ya pamoja ili kupata kiasi kikubwa cha korosho kwa wakati mmoja na kuongeza ajira kupitia kilimo hasa kwa vijana. Hadi sasa tumeanzisha mashamba hayo Manyoni na Lindi, vile vile tunataka kuanzisha shamba la hekari 1,000 wilayani Chunya”, alisema Kaimu Mkurugenzi Alfred.

Ameitaja mikoa ambayo inazalisha korosho kuwa ni Ruvuma, Mtwara, Lindi, Pwani, Tanga pamoja na mikoa mingine 12 ambayo imeshapandwa mazao lakini bado haijaanza uzalishaji ila imefanyiwa utafiti na kuaminiwa kuwa inaweza kuzalisha zao hilo.

Aidha, ametoa rai kwa wawekezaji kuongeza uwekezaji katika kununua mitambo ya kubangulia korosho kwani kati ya viwanda 52 vya kubangua korosho, ni viwanda kati ya 22 hadi 30 ndio vina mitambo ambayo ina uwezo wa kubangua korosho tani 64, 500 pekee kwa mwaka.

Amefafanua kuwa, kama viwanda vyote 52 vilivyopo vitawekewa mitambo ya ubanguaji, kwa mwaka uzalishaji wa zao hilo unaweza kufikia tani 185,000.    

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi