Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba ameihakikishia Denmark kwamba Tanzania iko tayari kushirikiana na nchi hiyo kupitia Mkakati wake mpya wa ushirikiano wa kimataifa kwa kuishirikisha sekta binafsi katika mipango yake ya maendeleo ili kukuza uchumi na ajira.
Dkt. Nchemba ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo na Sera za Mabadiliko ya Tabianchi wa Denmark, Mhe. Dan Jørgesen, jijini Dodoma.
Dkt. Nchemba alisema kuwa Tanzania ina fursa kubwa za uwekezaji katika sekta mbalimbali na kutoa wito kwa kampuni, mashirika na taasisi mbalimbali kutoka Denmark kushirikiana na sekta binafsi ya Tanzania kuwekeza mitaji na teknolojia ili pande zote mbili ziweze kunufaika.
Alisema kuwa mkazo mkubwa wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kuhakikisha kuwa sekta binafsi ndiyo inayotakiwa kuendesha uchumi wa nchi na kwamba ili kufanikisha mpango huo, Serikali imefanya mageuzi makubwa ya kisera na kisheria ili kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.
Dkt. Nchemba aliyataja baadhi ya maeneo yanayohitaji ushiriki wa sekta binafsi kuwa ni pamoja na uendeshaji wa reli ya kisasa ya SGR, masuala ya nishati, kilimo, na maeneo mengine kadha wa kadha.
Alisema kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana na Denmark kupitia mpango wake mpya wa ushirikiano baada ya kusitisha uamuzi huo wa kufunga ubalozi wake nchini ambapo nchi hiyo imepanga kuongeza kiwango cha ufadhili na kuelekeza fedha hizo kwenye maeneo yatakayokuza uchumi, ikiwemo nishati, kuboresha mifumo ya kodi, kilimo, elimu, afya, pamoja na kusaidia sekta binafsi.
Dkt. Nchemba alirejesha shukrani zake kwa Denmark kwa kuendeleza ushirikiano wake uliotimiza miaka 60, ambapo katika miaka ya hivi karibuni, nchi hizo mbili zilikuwa zikitekeleza miradi ambayo Denmark iliipatia Tanzania msaada wa takriban Denish Krone bilioni 2, sawa na shilingi za Tanzania bilioni 646.
Aidha, alisema kuwa Denmark kupitia Shirika lake la Maendeleo (DANIDA), imetoa zaidi ya shilingi bilioni 103 zinazotokana na mapato ya uwekezaji wake wa hisa katika Benki ya CRDB ambazo zimetumika kwa ajili ya kusaidia sekta ya afya kupitia Mfuko wa Afya.
Aliiomba pia Denmark kupitia Taasisi yake inayohusika na masuala ya Bima na Dhamana (Danish Export Credit Agency), kushiriki katika ujenzi wa mradi wa SGR kwa vipande vilivyobaki kutokana na umuhimu wa mradi huo katika kukuza biashara na ustawi wa maisha ya watu watakaotumia reli hiyo pamoja na kukuza pato la Taifa.
Kwa upande wake, Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo na Sera za Mabadiliko ya Tabianchi wa Denmark, Mhe. Dan Jørgesen, alimpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa hatua kubwa ambayo nchi imepiga kiuchumi licha ya ulimwengu kukabiliwa na changamoto mbalimbali na kwamba anaiona Tanzania kuwa moja ya nchi kubwa kiuchumi kwa siku zijazo.
Aliishauri Tanzania, kuishauri Denmark namna ya kuboresha ushirikiano na maeneo ya kimkakati ambayo nchi inataka kuyapa kipaumbele hususan katika eneo la uwekezaji na biashara katika mpango wake mpya wa ushirikiano na nchi za Afrika ambao nchi yake inauandaa na wanatarajia utazinduliwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amealikwa kuitembelea nchi hiyo.
Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Maendeleo wa Serikali ya Denmark, Mhe. Lotte Machon, Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mhe. Mette Dissing-Spandet, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, Balozi wa Tanzania katika nchi za Scandinavia, Dkt. Grace Olotu, na Balozi wa Tanzania wa Heshima nchini Denmark, Mhe. Simon Mears na Viongozi wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Serikali ya Denmark.